KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanya mauaji ya nguvu baada ya kuichapa JKT Tanzania mabao 6-1, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Huo ni ushindi wa pili wa kihistoria kwa Azam FC kwenye ligi ikishinda zaidi ya mabao matano, wa kwanza ukiwa ni ule waliipiga Villa Squad mabao 6-2 kwenye msimu wake wa kwanza Ligi Kuu 2008/2009.

Mara ya mwisho kupata ushindi mnono, ilikuwa ni msimu 2014/2015, ilipoichapa Mtibwa Sugar mabao 5-2 kwenye ligi, huku pia mwaka 2013 ikiichapa Al Nasr ya Juba kutoka Sudani Kusini 5-0 ugenini na kusonga mbele katika Kombe la Shirikisho Afrika kwa jumla ya mabao 8-1.

Kwa ushindi huo, Azam FC inafikisha jumla ya pointi 56 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, ikizidiwa pointi nane na Yanga iliyo kileleni kwa pointi 64.

Alikuwa ni nahodha Agrey Moris, aliyeiweka mbele Azam FC kwa bao la uongozi kwa kichwa dakika ya 15 akimalizia kona iliyochongwa na winga Enock Atta.

Dakika 10 baadaye, kiungo Mudathir Yahya, aliiongezea bao la pili kwa shuti zuri la chini akitumia vema pasi safi ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’, aliyeendelea kuwa kwenye ubora wake, kufanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa na uongozi wa mabao hayo.

Mabadiliko ya kipindi cha pili ya kuingia Donald Ngoma na kutoka Enock Atta, yaliongeza uhai zaidi kwenye eneo la ushambuliaji la Azam FC na kuweza kujipatoa mabao manne zaidi.

Dakika ya 60, Ngoma aliipatia bao la tatu Azam FC akifunga kufuatia krosi safi ya Mudathir, kabla ya Chirwa kutupia la nne dakika ya 73, akimalizia kwa kichwa krosi safi ya beki wa kushoto, Bruce Kangwa.

Ngoma alirejea tena nyavuni dakika ya 78 akifunga bao la kiufundi akiuzungusha mpira uliomshinda kipa JKT kufuatia pasi safi ya Domayo.

Lyanga aliyeingia dakika 13 za mwisho akichukua nafasi ya Joseph Mahundi, alihitimisha karamu hiyo ya mabao kwa Azam FC akipiga la sita kwa shuti la mbali akimalizia pasi ya Domayo dakika ya 88.

Bao pekee la JKT Tanzania limefungwa na Hassan Mwaterema dakika ya 80.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kukipiga dhidi ya Singida United, kwenye mchezo ujao wa ligi utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Machi 16 mwaka huu saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, David Mwantika, Agrey Moris (C), Stephan Kingue/Frank Domayo dk 71, Joseph Mahundi/Danny Lyanga dk dk 76, Mudathir Yahya, Obrey Chirwa, Salum Abubakar, Enock Atta/Donald Ngoma dk 55