IMESHAJULIKANA sasa kuwa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakutana na Kagera Sugar kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) ikifanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Kagera.

Droo ya hatua hiyo, nusu fainali na fainali imepangwa leo asubuhi kwenye ofisi za wadhamini wakuu wa michuano hiyo, Azam Media, ambapo mechi za robo fainali zitapigwa kati ya Machi 26 na 31 mwaka huu.

Mechi nyingine za robo fainali zitahusisha, KMC watakaochuana na African Lyon, Lipuli ikivaana na Singida United huku Alliance ikiikaribisha Yanga.

Azam FC ilitinga hatua hiyo baada ya kuifurusha nje Rhino Rangers ya Tabora mabao 3-0, huku awali ikizichapa Madini (2-0), Pamba (2-0), mechi zote zikifanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Hii ni mara ya kwanza kwa Azam FC kukutana na Kagera Sugar kwenye michuano hiyo, lakini utakuwa ni mchezo wa 22 wa mashindano kumenyana, katika mechi 21 zilizopita, Azam FC imeonekana kuwa na wastani mzuri ikiwa imeshinda mara 11, ikipoteza mara tano huku michezo mitano ikiisha kwa sare.

Aidha kama Azam FC ikifanikiwa kumtoa Kagera Sugar, itakata tiketi ya nusu fainali ikikutana na mshindi wa mechi kati KMC na African Lyon, ikipenya hapo tena ikatinga fainali kwa mara ya pili kwenye michuano hiyo, fainali itakayopigwa mkoani Lindi katika Uwanja wa Ilulu Juni Mosi mwaka huu.

Mara ya kwanza Azam FC kutinga fainali ya michuano hiyo ilikuwa ni msimu 2015/2016, ikipoteza dhidi ya Yanga kwa kufungwa mabao 3-1, bao la matajiri hao likiwekwa kimiani na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Didier Kavumbagu.

Mabingwa hao Kombe la Kagame na Mapinduzi Cup msimu huu, wamejiwekea malengo makubwa msimu huu ya kuhakikisha wanarejea kwenye michuano ya Afrika, ambapo kwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo itafanikiwa kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.