UONGOZI wa Azam FC, umetuma maombi kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya kutumia Uwanja wa Nyamagana katika mchezo wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Kagera Sugar utakaofanyika Aprili 3 mwaka huu.

Klabu hiyo Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, imechukua uamuzi huo kutokana na Uwanja wake wa nyumbani, Azam Complex kuwa mbioni kufungwa baada ya mchezo wake wa mwisho Machi 16 dhidi ya Singida United.

Uwanja huo unafungwa kupisha maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U-17) itakayofanyika nchini kuanzia Aprili 14-28, huku Uwanja wa Azam Complex ukiwa ndio uwanja utakaotumika kwa asilimia 95 ya mechi zote.

Azam FC inahamia Uwanja wa Nyamagana ulioko jijini Mwanza kucheza na Kagera Sugar, kutokana na uwanja huo kulingana na ule wa Azam Complex, huku pia Aprili 7 mwaka huu ikitakiwa kucheza mchezo mwingine jijini humo dhidi ya Mbao utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba saa 10.00 jioni.