KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeendelea kufanya kweli baada ya kuichapa African Lyon mabao 3-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam leo jioni.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 53 ikibakia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, ikizidiwa pointi nane na kinara Yanga mwenye pointi 61 huku akiwa na mchezo mmoja mkononi, Simba iliyocheza mechi 19 ikiwa nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia 48.

Azam FC ilianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la uongozi dakika ya sita lililofungwa na mshambuliaji, Obrey Chirwa, akitumia vema pasi ya winga Ramadhan Singano ‘Messi’, aliyewapiga chenga mabeki kabla ya kutoa pande hilo.

Dakika tisa baadaye Lyon ilisawazisha kupitia kwa Baraka Jaffary, akiunganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na Polland Msonjo, bao lililofanya kipindi cha kwanza kumalizika kwa sare hiyo.

Kipindi cha pili Azam FC ilirejea na kasi mpya baada ya mabadiliko ya kuingia mshambuliaji Donald Ngoma na kiungo Stephan Kingue, na kufanikiwa kupata mabao mawili yaliyoamua ushindi wao katika mchezo huo.

Alikuwa ni kiungo Mudathir Yahya, aliyeiweka mbele Azam FC kwa bao safi la pili dakika ya 65, akifunga kwa shuti kali nje ya eneo la 18 baada ya kuunasa mpira uliookolewa vibaya na mabeki kufuatia krosi safi ya beki wa kulia, Nickolas Wadada.

Wakati watu wakidhani mchezo ungemalizika kwa ushindi huo, mambo yalibadilika dakika ya 90, baada ya beki wa kushoto wa Azam FC, Bruce Kangwa, kuwachachafya mabeki wa Lyon na kupiga krosi nzuri ya chini iliyopelekea beki wa Lyon, Msonjo kujifunga wakati akiwa kwenye hatari ya kuokoa.

Ushindi huo unaondoa matokeo mabaya ya Azam FC yaliyokuwa yametawala kwenye mechi tano zilizopita za ligi, ambapo huo ni ushindi wa kwanza baada ya mechi hizo, ndani ya mechi hizo ilikuwa imepoteza mara mbili na kutoka sare tatu.

Aidha huo ulikuwa mchezo wa pili mfululizo kwa Azam FC kuibuka kidedea ikiwa na benchi jipya la ufundi la muda chini ya makocha Idd Nassor Cheche na Meja Mstaafu Abdul Mingange, baada ya awali kushinda mechi yao ya kwanza iliyokuwa ya Kombe la FA, Azam ikiichapa Rhino Rangers 3-1.

Makocha hao wameshika nafasi hizo baada ya uongozi wa timu hiyo kusitisha mikataba ya Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi, kufuatia matokeo mabaya yaliyokuwa yakiiandama timu hiyo kwenye mechi tano zilipita kabla ya kucheza na Rhino Rangers.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, David Mwantika, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya, Salum Abubakar, Frank Domayo/Stephan Kingue dk 46, Obrey Chirwa, Tafadzwa Kutinyu/Donald Ngoma dk 46, Ramadhan Singano/Danny Lyanga dk 67