KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa na kibarua kingine cha mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) pale itakapovaana na African Lyon, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kesho Ijumaa saa 10.00 jioni.

Azam FC inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kuichapa Rhino Rangers mabao 3-0 na kusonga mbele kwa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).
Kikosi hicho kilirejea mazoezini tokea jana, tayari kujiweka sawa na mchezo huo unaotarajia kuwa na mkali na wa aina yake kutokana na uhasimu wa timu zote mbili zinazotokea eneo moja, Azam FC ikitokea Chamazi na Lyon ikiwa na makazi yake Mbagala.

Kwa mara nyingine katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaongozwa na makocha wa muda, Idd Nassor Cheche na Meja Mstaafu, Abdul Mingange, walioanza kibarua chao tokea mchezo uliopita walipoichakaza Rangers.

Morali ya wachezaji ipo juu tayari kufanikisha ushindi muhimu katika mchezo huo wa kwanza kwa timu hiyo mwezi Machi mwaka huu, ambapo benchi la ufundi limekuwa likifanya kazi kubwa ya kuwajenga vijana kimbinu na kisaikolojia.

Mabingwa hao wa ligi msimu 2013/2014, ikilitwaa bila kupoteza mchezo wowote, walifanikiwa kuiadabisha Lyon kwenye mchezo wa raundi ya kwanza uliofanyika Uwanja wa Azam Complex mwaka jana, Azam FC ikishinda mabao 2-1.

Mabao ya Azam FC yaliwekwa kimiani na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Yahya Zayd, aliyetimkia Ismaily ya Misri, huku la pili likifungwa na beki Abdallah Kheri, akimalizia mpira wa kona uliochongwa na Zayd na kuokolewa vibaya na mabeki kabla ya mfungaji kuusukumizia mpira nyavuni.

Aidha kihistoria timu hizo zimekutana mara 11 kwenye mechi za ligi, Azam FC ikiwa imeshinda mechi saba, sare tatu na kupoteza mmoja, huku jumla ya mabao 26 yakiwa yamewekwa kimiani katika michezo yote hiyo, matajiri hao wakizitungua nyavu za wapinzani wao mara 18 na Lyon ikiziona nyavu za Azam FC mara nane.

Ushindi wowote wa Azam FC kesho utaifanya kufikisha pointi 53 na kujikita zaidi nafasi ya pili kwenye msimamo huku ikiisogelea zaidi Yanga iliyokuwa nazo 61, huku Simba iliyocheza mechi 19 ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi zake 48.