KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetinga robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya kuichapa Rhino Rangers mabao 3-0, mchezo uliomalizika usiku huu kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na benchi jipya la ufundi, likiwa na makocha wazawa wa muda, Idd Nassor Cheche na Meja Mstaafu, Abdul Mingange, ambao wanafundisha pia timu za vijana za timu hiyo.

Wawili hao wameshika nafasi hizo baada ya kusitishiwa kwa mikataba kwa makocha Hans Van Der Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi, wikiendi iliyopita.

Mabingwa hao waliingia na morali kubwa kwenye mchezo na dakika ya 10 tu walifanya shambulizi kali, ambapo shuti lililopigwa na kiungo mshambuliaji, Tafadzwa Kutinyu, liligonga mwamba.

Dakika 10 baadaye Kutinyu alirekebisha makosa yake, na kuipa bao la uongozi Azam FC akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Rhino Rangers kufuatia shuti la nahodha Agrey Moris.

Bao hilo lilidumu hadi kumalizika kwa kipindi cha kwanza, na kipindi cha pili Azam FC iliingia na kasi mpya ikicheza soka la pasi ikichanganya na mipira mirefu.

Dakika ya 55 kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, aliyekuwa kwenye kiwango bora, aliipatia bao la pili Azam FC kwa shuti akimalizia kazi nzuri ya mshambuliaji Obrey Chirwa.

Chirwa alihitimisha ushindi huo mnono wa Azam FC kwa kuipatia bao la tatu dakika ya 68, akifunga kwa staili ya kuubetua mpira, alioupata baada ya kuokolewa vibaya na beki aliyekuwa akiwani mpira na winga wa Enock Atta.

Azam FC kwa kufuzu hatua hiyo, sasa huenda ikakutana na timu nyingine saba zilizofuzu hatua hiyo, Lipuli, Yanga, Kagera Sugar, KMC, Alliance, Singida United na African Lyon.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kurejea mazoezini keshokutwa Jumatano, kujiandaa na maandalizi ya mechi ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya African Lyon utakaofanyika Ijumaa hii.

Bingwa wa michuano hiyo, anatarajia kuiwakilisha Tanzania Bara kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, itakayoanza kutimua vumbi katika hatua ya mtoano kuanzia Novemba mwaka huu.S

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Agrey Moris (C), Yakubu Mohammed, Mudathir Yahya, Joseph Mahundi/Frank Domayo dk 74, Salum Abubakar, Obrey Chirwa, Tafadzwa Kutinyu/Enock Atta dk 60, Ramadhan Singano/Donald Ngoma dk 57