KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itashuka dimbani kusaka robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) ikivaana na Rhino Rangers ya Tabora kwenye Uwanja wa Azam Complex kesho Jumatatu saa 1.00 usiku.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na benchi jipya la ufundi chini ya makocha wa muda, Meja Mstaafu, Abdul Mingange na Idd Nassor Cheche, wanaofundisha timu za vijana za timu hiyo, na hii ni baada ya jana kusitishiwa mikataba kwa makocha waliopita, Hans Van Der Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi.

Wachezaji wa timu hiyo wako na morali nzuri kuelekea mchezo huo na usiku huu wamefanya mazoezi ya mwisho, kila mchezaji akiwa fiti tayari kwa mapambano ya dakika 90 kuhakikisha Azam FC inasonga kwa raundi ijayo ya robo fainali utakayoshirikisha timu nane bora.

Mabingwa hao waliingia raundi ya 16 bora baada ya kuichapa Pamba ya Mwanza mabao 2-0, yaliyofungwa na winga machachari Ramadhan Singano ‘Messi’ na kabla ya hapo ilipata ushindi kama huo dhidi ya Madini ya Arusha, kwa mabao safi ya Enock Atta na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Yahya Zayd, aliyetimkia Ismaily ya Misri.

Rangers ambayo ni timu ya jeshi, ilifika hatua hiyo baada ya kuiondoa mashindanoni Stand United ikiipiga bao 1-0 mchezo uliopigwa mjini Tabora.

Huo utakuwa ni mchezo wa tatu kwa timu hizo kukutana kwenye mashindano mbalimbali, mara mbili za awali zilikutana kwenye ligi msimu wa 2013/2014 kabla ya Rangers kushuka daraja kwenye msimu wake huo wa kwanza ndani ya ligi, Azam FC ikishinda zote mbili, ugenini ikiichapa 2-0 na nyumbani ikaibuka kidedea 1-0.

Wababe hao kutoka viunga vya Azam Complex waliolikosa taji hilo mara tatu tokea lirejeshwe tena na TFF mwaka 2015, wamejipanga kutwaa ubingwa huo msimu huu, ili kurejea kwenye michuano ya kimataifa, kwani bingwa ataweza kuiwakilisha Tanzania Bara katika Kombe la Shirikisho Afrika baadaye mwishoni mwa mwaka huu.