UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, unatangaza kuachana na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hans Van Der Pluijm baada ya kufikia makubaliano ya pande zote mbili.

Azam FC imefikia makubaliano ya kuachana na Mholanzi sambamba na Msaidizi wake, Juma Mwambusi, kutokana na kutoridhishwa na matokeo ya hivi karibuni kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).

Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo sambamba na uongozi mzima unashukuru mchango mkubwa wa makocha hao walioutoa kwa Azam FC kwa kipindi chote walichotoa huduma ndani ya timu hiyo na unawatakia kila la kheri katika maisha yao mapya ya soka.

Kutokana na mabadiliko hayo ya haraka, kwa sasa benchi la ufundi la Azam FC litasimamiwa kwa muda na makocha wa timu za vijana za timu hiyo, Meja Mstaafu Abdul Mingange (Azam U-20) na Idd Nassor Cheche (Azam U-17).

Aidha kwa sasa uongozi wa timu hiyo upo kwenye mchakato wa kutafuta kocha atayerithi mikoba ya Pluijm, na mara taratibu zote zitakapokamilika tutatoa taarifa rasmi.