NAHODHA Msaidizi wa Azam FC, Frank Domayo ‘Chumvi’, amesema kuwa mara baada ya kurejea dimbani, jambo muhimu hivi sasa ni kupambana akishirikiana na wachezaji wenzake na kuipa matokeo ya ushindi timu hiyo kwa mechi zilizobakia.

Domayo amerejea dimbani jana wakati Azam FC ikipoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Simba, baada ya kukaa nje ya dimba kwa muda wa miezi minne akiuguza majeraha ya goti, aliingia uwanjani dakika ya 67 kuchukua nafasi ya Joseph Mahundi, na kufunga bao pekee la timu yake.

Kiungo huyo ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa anajisikia furaha kurejea tena dimbani huku akitoa shukrani kubwa kwa viongozi wa timu hiyo na wachezaji wenzake kwa kumpa ushirikiano kwa kipindi chote alichokuwa nje ya dimba.

“Kwanza namshukuru Mungu kwa kupona pia naushukuru uongozi wa Azam FC na wachezaji kwa ujumla kwa kunipa sapoti wakati nipo nje ya dimba, pia nilivyorudi jana dhidi ya Simba nashukuru nimecheza na kufunga ni kitu kizuri lakini kikubwa ni kupona na kuwa fiti kwa ajili ya kuisaidia timu,” alisema.

Kiungo huyo nyota aliyekuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, aliwaomba mashabiki wa timu hiyo waendelee kuisapoti timu hiyo licha ya hivi karibuni kutopata matokeo waliyotarajia.

“Tunawaomba radhi mashabiki kwa matokeo ya hivi karibuni, tunapitia kipindi cha mpito hivi sasa, tutarejea kwenye hali yetu ya kawaida kama mwanzo, cha muhimu kilichobakia kwetu hivi sasa ni kufanya vizuri kila mechi na kupata matokeo mazuri,” alisema.