KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeteleza kwenye muendelezo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) baada ya kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Simba.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kubakiwa na pointi zake 50 katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, ikizidiwa pointi 11 na Yanga iliyonafasi ya kwanza huku Simba iliyocheza mechi 18 ikiwa nafasi ya tatu baada ya kujizolea pointi 45.

Simba ilitangulia kupata bao la uongozi dakika ya tano likifungwa na mshambuliaji Meddie Kagere, kabla ya nahodha wa zamani wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, kufunga la pili dakika ya 39 akimalizia kwa kichwa krosi ya Zana Coulibaly.

Azam FC ambayo ilitawala mchezo huo dakika 20 za mwisho za kipindi cha kwanza, ingeweza kusawazisha mabao hayo kama ingetumia vema nafasi walizopata kupitia mshambuliaji Obrey Chirwa na ile ya kiungo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, aliyepiga shuti zuri lililogonga mwamba kabla ya mpira kuokolewa na mabeki.

Kipindi cha pili Azam FC iliendelea na kasi yake na dakika ya 46 mshambuliaji Donald Ngoma, alikosa nafasi ya wazi wakati akitazamana na kipa wa Simba, Aishi Manula, baada ya kupiga shuti lililopaa juu ya lango.

Simba ikajipatia bao la tatu dakika ya 77, lililofungwa tena na Kagere akimalizia pasi ya, Clatous Chama aliyegongeana na kiungo mwenzake, Muzamiru Yassin.

Kiungo Frank Domayo, aliyekuwa nje ya dimba kwa muda wa miezi minne, aliyerejea kwenye mchezo huo akiingia dakika ya 67 kuchukua nafasi ya winga Joseph Mahundi, aliipatia bao la kufuatia machozi Azam FC dakika ya 81 kwa shuti kali nje ya eneo la 18 akimalizia pasi safi ya Ngoma.

Dakika ya 85 mwamuzi wa mchezo huo, Kheri Sasii, alikataa bao lililofungwa na beki Agrey Moris kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na beki, Bruce Kangwa, akidai alitumia mabega ya Kagere wakati akipiga kichwa hiko.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Rhino Rangers, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex keshokutwa Jumatatu saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya, Joseph Mahundi/Frank Domayo dk 67, Tafadzwa Kutinyu/Donald Ngoma dk 46, Obrey Chirwa, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Ramadhan Singano/Enock Atta dk 46.