KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa kibaruani kuvaana na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho Ijumaa saa 10.00 jioni.

Kikosi cha Azam FC kinamorali ya juu kuelekea mchezo huo, wachezaji wote wakionekana kuwa fiti kwa ajili ya kupambana kuzoa pointi zote tatu na kuendelea na vita ya kuwania taji la ligi hiyo.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Coastal Union, katika mchezo uliopita wa ligi huku Simba ikitoka kushinda mabao 3-0 walipovaana na African Lyon.

Nahodha wa Azam FC, Agrey Moris, atakuwa akirejea dimbani kuimarisha safu ya ulinzi, baada ya kuukosa mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union, akitumikia adhabu ya kukusanya kadi tatu za njano.

Huo utakuwa ni mchezo wa kwanza wa ligi kwa timu hizo kukutana msimu huu, na wa pili kwenye mashindano yote, kwani Januari 13 mwaka huu zilikutana katika fainali ya Kombe la Mapinduzi na Azam FC kuibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-1, yaliyofungwa na kiungo Mudathir Yahya na mshambuliaji Obrey Chirwa.

Kihistoria timu hizo zimekutana mara 20 kwenye mechi za ligi tokea Azam FC ipande daraja msimu wa 2008/2009, matajiri hao wakishinda mara tano, Simba wakiibuka kidedea mara tisa na ikishuhudiwa mechi sita wakienda sare.

Aidha kwenye mechi za mashindano yote zimekutana mara 31, Azam FC ikishinda mara 12, Simba mara 13 huku mechi sita zikienda sare, hiyo inajumuisha mechi za ligi, Kombe la Mapinduzi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), Kombe la Kagame, Kombe la Ujirani Mwema, Kombe la Banc ABC Super 8 na Ngao ya Jamii.

Hadi hivi sasa msimu huu, Azam FC imejikusanyia pointi 50, ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 24 za ligi, ikishinda mara 14, sare nane na kupoteza mechi mbili, Simba iliyonafasi ya tatu imecheza mechi 17, imeshinda 13, sare tatu na kupoteza moja ikijikusanyia pointi 42.