KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union ugenini, mchezo uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Sare hiyo inaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 50 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikizidiwa pointi nane na Yanga iliyojikusanyia pointi 58 kileleni.

Coastal Union ndio iliyoanza kupata bao la uongozi dakika ya 45 likifungwa na Ayoub Lyanga, akitumia uzembe wa safu ya ulinzi bao lililodumu hadi kumalizika kwa kipindi cha kwanza.

Azam FC ilianza vema kipindi cha pili kwa kufanya mashmbulizi mfululizo, jitihada zilizozaa matunda dakika ya 52 kwa kupata bao la kusawazisha lililofungwa na mshambuliaji, Obrey Chirwa, aliyemalizia mpira uliotemwa na kipa kufuatia shuti la Tafadzwa Kutinyu.

Dakika za mwisho kiungo Mudathir Yahya, alishindwa kutumia vema nafasi nzuri aliyopata akilitizama lango la Coastal baada ya kuupiga vibaya mpira na kupaa juu ya lango.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka jijini Tanga kesho Jumatano alfajiri kurejea jijini Dar es Salaam tayari kwa maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Simba, utakofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam Ijumaa hii.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed (C), Stephan Kingue/Mudathir Yahya dk 66, Joseph Mahundi, Salum Abubakar, Obrey Chirwa, Tafadzwa Kutinyu/Idd Kipagwile dk 70, Ramadhan Singano/Donald Ngoma dk 61