KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa kibaruani ugenini kupambana na Coastal Union, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) unaotarajia kufanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kesho Jumanne saa 10.00 jioni.

Kikosi cha Azam FC kimeshawasili mkoani Tanga leo Jumatatu mchana tayari kabisa kwa mchezo, wachezaji wakiwa wamejiandaa vema kwa ajili ya kufanikisha lengo la kusaka pointi tatu muhimu katika mchezo huo.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi iliyopita baada ya kufungwa na Tanzania Prisons bao 1-0 ugenini, huku Coastal Union ikitoka kupigwa 2-1 na Mwadui.

Benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Mholanzi, Hans Van Der Pluijm, limejiwekea mipango ya ushindi kwenye mchezo huo ambapo kila mara wamekuwa wakiwasisitiza wachezaji kujitahidi kufanya kweli kutokana na umuhimu wa mtanange huo.

Eneo la langoni la Azam FC, litaimarika kwa kurejea kipa Razak Abalora, aliyekosa mechi mbili zilizopita akitumikia adhabu ya kadi nyekundu, ambapo nafasi yake ilizibwa vema na Benedict Haule, aliyeonekana kucheza vema katika milingoti hiyo mitatu.

Nahodha wa Azam FC, Agrey Moris, atakosekana kwenye mchezo huo akitumikia adhabu ya kukosa mechi moja baada ya kukusanya kadi tatu za njano na aanatarajia kurejea fiti kabisa katika mchezo wetu ujao dhidi ya Simba, utakaofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam Ijumaa hii.

Itakumbukwa kuwa katika mchezo wa raundi ya kwanza timu hizo zilipokutana Uwanja wa Azam Complex, Azam FC ilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na washambuliaji wake, Donald Ngoma na Danny Lyanga, kwenye mchezo uliokuwa mkali na wa aina yake.

Kuelekea mchezo huo, kitakwimu Azam FC ina rekodi nzuri dhidi ya Wagosi wa Kaya hao kwani katika mechi zote 11 walizokutana kwenye ligi, Azam FC imeshida nane, ikiwa imepoteza moja na mbili zikiisha kwa sare.

Katika mechi zote hizo 11 jumla ya mabao 24 yamefungwa, ambapo Azam FC imefunga asilimia 98 ya mabao yote ikitupia 20 na Coastal ikifunga manne pekee.  

Ushindi wowote kwa Azam FC kesho utaifanya kuzidi kujiweka sawa kwenye msimamo wa ligi, kwani hadi sasa imefanikiwa kujikusanyia pointi 49 katika nafasi ya pili ikizidiwa pointi tisa na vinara Yanga wenye 58 lakini wakiwa wamecheza mechi moja zaidi dhidi ya matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex.