KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imepoteza mechi ya pili kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) baada ya kufungwa na Tanzania Prisons bao 1-0.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kubakiwa na pointi zake 49 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo, ikizidiwa pointi tisa na vinara Yanga waliokuwa nazo 58.

Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Sokoine, Mbeya ulikuwa ni mkali na wa aina yake, Azam FC ikionekana kutengeneza nafasi kadhaa lakini ikashindwa kuzitumia kwa kupata mabao.

Bao pekee la Prisons limefungwa kwa mkwaju wa penalti dakika ya 35 na nahodha wa timu hiyo, Jumanne Elfadhili, iliyotokana na beki Yakubu Mohammed, kugongwa na mpira mkononi na mwamuzi kuamuru penalti.

Azam FC iliweza kucheza vema kipindi cha pili na kupata nafasi mbili muhimu za kujipatia mabao, moja ikiwa ni shuti lililopigwa na kiungo Mudathir Yahya, kugonga mwamba wa juu kabla ya mpira kuokolewa na mabeki.

Nafasi nyingine na kichwa safi kilichopigwa na beki Yakubu, lakini kipa wa Prisons, Aron Kalambo, alichumpa na kuundoa mpira uliokuwa ukielekea wavuni na kuinyima Azam FC nafasi ya kusawazisha bao hilo.

Huo unakuwa ni mchezo wa pili kwa Azam FC kupoteza msimu huu, yote ikiwa ni ya ugenini, wa kwanza ulikuwa kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro, ikiteleza na kufungwa na Mtibwa Sugar mabao 2-0.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho Ijumaa alfajiri, ambapo mara moja kitaanza maandalizi ya mtanange mwingine wa ugenini dhidi ya Coastal Union utakaofanyika Uwanja wa Mkwakwani Februari 19 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC:

Benedict Haule, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya, Obrey Chirwa, Salum Abubakar/Idd Kipagwile dk 85, Donald Ngoma/Danny Lyanga dk 72, Tafadzwa Kutinyu, Ramadhan Singano/Joseph Mahundi dk 75