KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, tayari kimewasili salama mkoani Mbeya kikiwa kimejidhatiti kufanya kweli kwenye mchezo ujao dhidi ya Tanzania Prisons.

Azam FC inawasili mkoani humo ikiwa imetoka kucheza mkoani Iringa dhidi ya Lipuli jana Jumatatu, ikipata sare ya bao 1-1 huku bao lake likifungwa na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Msaidizi wa Azam FC, Juma Mwambusi, aliwapongeza wachezaji kwa kutoka nyuma na hatimaye kupata sare ya ugenini.

“Mchezo ulikuwa ni mzuri na mgumu, Azam kipindi cha kwanza hatukuweza kucheza vizuri kwa sababu wachezaji waliingia kwenye mchezo wakiwa na kasi ya chini, kwa kiasi kikubwa ilichangiwa na hali ya uwanja kwa sababu ilinyesha mvua kabla ya mpira kuanza kwa hiyo walicheza kwa tahadhari zaidi ili wasiweze kupata majeraha na kusababisha matatizo langoni,” alisema.

Alisema waliweza kufanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kucheza mpira wa kushambulia kutokea pembeni na katikati hadi kufanikiwa kusawazisha bao wailotanguliwa kipindi cha kwanza na Lipuli.

“Pengine tungeweza kutulia zaidi kwa washambuliaji wetu tungeweza kushinda mabao mawili au matatu na kuondoka na pointi tatu katika mechi hii, yote kwa yote tunajipanga kwa mchezo unaokuja (Tanzania Prisons,” alisema.

Mara baada ya kikosi cha Azam FC kuwasili mkoani Mbeya, kesho Jumatano kinatarajia kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Sokoine kabla ya kuvaana na maafande hao.

Matokeo ya jana yameifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 49 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikizidiwa pointi tisa na vinara Yanga waliokuwa nazo 58, lakini matajiri hao wakiwa na mchezo mmoja mkononi.