BAO lililofungwa na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy, limeiwezesha Azam FC kupata sare ya 1-1 ugenini dhidi Lipuli, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Samora mkoani Iringa.

Azam FC kwa kupata sare hiyo hivi sasa wanafikisha jumla ya pointi 49 katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikizidiwa pointi tisa na Yanga iliyokuwa nazo 58.

Kipa wa Azam FC, Benedict Haule, aliweza kusimama imara langoni ikiwa ni mechi yake ya kwanza ya ligi kucheza msimu huu, akiokoa michomo kadhaa ya washambuliaji wa Lipuli.

Lipuli ilianza kupata bao la uongozi dakika ya 45 lililofungwa kwa kichwa na Daruwesh Saliboko, na kupelekea mpira kwenda mapumziko kwa uongozi wa Wanapaluhengo hao.

Kipindi cha pili Azam FC ilionekana kucheza vizuri tofauti na kipindi cha kwanza, ambapo ilifanya shambulizi kali dakika ya 47 lakini pasi safi ya Donald Ngoma, ilishindwa kumfikia Obrey Chirwa, aliyekuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga kufuatia mabeki wa Lipuli kuokoa hatari hiyo.

Dakika chache baadaye Chirwa alikosa nafasi ya wazi, akiwa amefanikiwa kuihadaa safu ya ulinzi ya Lipuli, lakini shuti alilopiga lilitoka pembeni kidogo ya lango la Lipuli.

Kuingia kwa viungo washambuliaji, Joseph Mahundi na Tafadzwa Kutinyu, kipindi cha pili katikati kuliongeza kasi ya mashambulizi na hatimaye Azam FC kupata bao hilo la kusawazisha dakika ya 81, lililofungwa na Sure Boy kwa shuti zuri akimalizia pasi ya Ngoma, aliyepokea pande zuri kutoka kwa Kutinyu.

Matokeo hayo yanazidi kuonyesha upinzani mkali baina ya timu hizo tokea zilipoanza kukutana mara baada ya Lipuli kupanda daraja msimu uliopita, katika mechi nne walizokutana, Azam FC imeshinda mmoja na nyingine tatu zikienda sare.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka mjini Iringa kesho Jumanne asubuhi tayari kwa safari ya kuelekea mkoani Mbeya kukipiga na Tanzania Prisons Februari 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine.

Kikosi cha Azam FC:

Benedict Haule, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Stephan Kingue/Joseph Mahundi dk 57, Obrey Chirwa, Mudathir Yahya, Donald Ngoma, Salum Abubakar/Idd Kipagwile dk 90, Ramadhan Singano/Tafadzwa Kutinyu 67