KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa ugenini kesho Jumatatu kuvaana na Lipuli katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Samoro mkoani Iringa.

Kikosi cha Azam FC tayari kimewasili salama mkoani Iringa usiku wa jana, kikiwa na ari kubwa ya kupata ushindi, wachezaji wote wakiwa kwenye hali nzuri kabisa kiafya na kupambana kwa ajili ya mchezo huo muhimu.

Azam FC itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Alliance kwenye mchezo uliopita wa ligi uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, huku Lipuli ikitoka kushinda bao 1-0 ilipochuana na KMC nyumbani mjini Iringa.

Timu zote mbili zimeonekana kuwa kwenye nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi, Azam FC ikiwa nafasi ya pili kwa pointi zake 48 huku Lipuli ikiwa nafasi ya nne baada ya kujisanyia pointi 36.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, anataka kuhakikisha kuwa anafanikiwa kupata pointi tatu kwenye mchezo huo na mara kwa mara amekuwa akiwasisitiza wachezaji juu ya umuhimu wa kupata matokeo ya ushindi dhidi ya Wanapaluhengo hao, ili kuendelea na mbio za kuwania ubingwa.

Azam FC itamkosa kipa wake namba moja, Razak Abalora, ambaye alipewa kadi nyekundu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Alliance, hivyo itakuwa nafasi kwa makipa waliobakia kikosini kuweza kuziba nafasi hiyo katika mechi zijazo atakazokosekana.

Hii ni mara ya nne timu hizo kukutana kihistoria kwenye mechi za ligi, katika mechi tatu za awali zilizopita Azam FC imeshinda mara moja huku mechi mbili wakienda sare, mara ya mwisho kukutana kwenye uwanja huo zilitoka suluhu, huku suluhu nyingine ikiwa ni msimu huu zilipokutana katika raundi ya kwanza.