KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, tayari kimewasili salama mkoani Iringa usiku huu kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Lipuli.

Mchezo huo unatarajia kufanyika Uwanja wa Samora mkoani humo keshokutwa Jumatatu, Azam FC ikiwa imejipanga vema kupata matokeo mazuri kwenye mtanange huo muhimu kabisa katika mbio zake za kuwania taji la ligi hiyo.

Baada ya kuwasili kikosi hicho, kesho Jumapili kinatarajia kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja huo itakaochezea mechi, tayari kusuka mipango ya mwisho ya kiufundi kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.

Msafara wa Azam FC, uliokuwa ukiongozwa na Meneja wa timu, Phillip Alando, umewasili ukiwa na jumla ya wachezaji 21 wakiwemo makocha wakiongozwa na Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi na Kocha wa makipa, Idd Abubakar na daktari wa timu, Mwanandi Mwankemwa.

Wachezaji wanaoundwa na makipa Mwadini Ally, Benedict Haule, Wilbol Maseke, mabeki ni nahodha Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Bruce Kangwa, Nickolas Wadada, David Mwantika, Lusajo Mwaikenda, Hassan Mwasapili.

Viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya, Stephan Kingue, Tafadzwa Kutinyu, Salmin Hoza, mawinga Joseph Mahundi, Ramadhan Singano ‘Messi’, Idd Kipagwile na washambuliaji ni Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Danny Lyanga.

Timu hizo zilipokutana raundi ya kwanza kwenye Uwanja wa Azam Complex, zilitoka suluhu ya bila kufungana, Azam FC ikionekana kucheza soka la hali ya juu lakini ilikosa bahati ya ushindi kufuatia kukosa nafasi kadhaa za kufunga.