KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa nje ya jiji la Dar es Salaam kwa wiki moja ikihamishia vita yake ya kuwania pointi sita kwenye mikoa miwili ya Nyanda za Juu kuanzia kesho Jumamosi.

Azam FC inatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam kesho Jumamosi Alfajiri tayari kwa safari hiyo, ikielekea mkoani Iringa itakapochuana na Lipuli kwenye Uwanja wa Samora jijini humo Jumatatu ijayo kabla ya Februari 12 kuelekea mkoani Mbeya kukipiga na Tanzania Prisons Februari 14.

Kikosi cha Azam FC kipo katika hali nzuri, kikitarajia kufanya mazoezi mwisho jijini Dar es Salaam leo Ijumaa jioni kabla ya kuelekea kwenye mikoa hiyo ya Nyanda za Juu, ambapo malengo makuu ni kuhakikisha inapata matokeo mazuri kabisa.

Mabingwa hao wanaelekea kucheza na Lipuli wakiwa na kumbumbuku ya kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani kwenye mchezo uliopita dhidi ya Alliance, ambao walisawazisha dakika za mwisho kwa bao lililokuwa na utata, kufuatia nahodha wa Azam FC, Agrey Moris, kufanyiwa madhambi kabla ya mfungaji, Dickson Ambundo, kuuweka mpira wavuni.

Kipa wa Azam FC, Razak Abalora, atakosekana kwenye mchezo huo baada ya kupata kadi nyekundu katika wakati akipinga maamuzi ya mwamuzi msaidizi namba moja, Mohamed Mkono (Tanga), aliyeruhusu bao hilo licha ya madhambi yaliyofanyika.

Kukosekana na Abalora kutafungua milango kwa makipa wengine kikosini, Mwadini Ally na Benedict Haule, kuipigania Azam FC katika mechi zijazo muhimu itakazocheza ugenini kabla ya kurejea Dar es Salaam kuvaana na Simba.

Aidha Azam FC itanufaika na urejeo wa beki wake mahiri wa kushoto, Bruce Kangwa, ambaye alikosekana kwenye mchezo uliopita baada ya kupewa ruhusa maalumu ya kwenda nchini kwao Zimbabwe, kushughulikia matatizo binafsi ya kifamilia.

Wababe hao kutoka viunga vya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, hadi sasa wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na pointi 48 ikizidiwa pointi saba na vinara Yanga waliofikisha 55, lakini matajiri hao wakiwa na mchezo mmoja mkononi.