KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imelazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Alliance katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Sare hiyo inaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 48 katika nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na mchezo mmoja mkononi, ikizidiwa pointi saba na kinara Yanga aliyefikisha 55 kufuatia suluhu yake ya jana dhidi ya Singida United.

Mchezo huo ulikuwa na kasi sana, Azam FC ikianza kwa mashambulizi makali langoni mwa Alliance, ambapo dakika ya kwanza Obrey Chirwa, alikosa bao la wazi baada ya kuupiga vibaya mpira akiwa anatazamana na lango ndani ya eneo la hatari, akipokea pasi ya Donald Ngoma.

Mabingwa hao waliweza kupata ugumu kuipenya safu ya ulinzi ya Alliance, kutokana na timu hiyo kusimama wengi kujilinda nyuma ya mpira wakati Azam FC ikishambulia.

Ilibidi Azam FC iweze kusubiri hadi dakika ya 79 kuweza kupata bao la uongozi, lililofungwa na Joseph Mahundi, aliyeingia dakika ya 76, kuchukua nafasi ya Ramadhan Singano, na alifunga bao hilo kiustadi akiunganisha krosi ya Chirwa.

Dakika ya 90 Alliance ilisawazisha kupitia kwa Dickson Ambundo, akimalizia mpira uliogonga mwamba kufuatia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Israel Patrick.

Lakini bao hilo limeonekana kuwa utata mkubwa kutokana na nahodha wa Azam FC, Agrey Moris, kusukumwa na Bigirimana Blaise, wakati akijaribu kuokoa mpira uliogonga mwamba na mpira kumgonga mfungaji Ambundo na kujaa wavuni.

Licha ya Moris kufanyiwa tukio hilo, mwamuzi Abubakar Mturo (Mtwara) na Msaidizi namba moja, Mohamed Mkono (Tanga), walishindwa kuliona na kuamuru kuwa bao halali, ambalo lililalamikiwa na wachezaji wa Azam FC.

Mara baada ya mchezo huo kumalizika, kipa wa Azam FC, Razak Abalora, alionyeshwa kadi nyekundu ya kufuatia kutoridhishwa na maamuzi ya mwamuzi huyo.

Mabingwa hao wa ligi msimu 2013/2014, wanatarajia kucheza mechi tatu zijazo ugenini, wakianza mkoani Iringa kukipiga na Lipuli Februari 11, kabla ya kumenyana na Tanzania Prisons mkoani Mbeya siku tatu baadaye na kumaliza na Coastal Union jijini Tanga, Februari 19 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Hassan Mwasapili, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Stephan Kingue, Obrey Chirwa, Mudathir Yahya, Donald Ngoma/Danny Lyanga dk 85, Salum Abubakar, Ramadhan Singano/Joseph Mahundi dk 76