KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuufungua mwezi Februari kwa kuvaana na Alliance katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Jumatano saa 2.00 usiku.

Azam FC inaendelea vema na maandalizi kuelekea mchezo huo, ambapo wachezaji wote wako kwenye hali nzuri tayari kwa mapambano ya kuwania pointi tatu muhimu ili kuendelea na kasi ya kufukuzia ubingwa wa ligi hiyo.

Mabingwa hao watashuka dimbani wakitoka kuichapa Biashara United mabao 2-1 kwenye mchezo uliopita wa ligi huku Alliance nayo ikiifunga Lipuli ya Iringa 2-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.  

Hii ni mara ya pili kwa timu hizo kukutana na kihistoria tokea Alliance ipande daraja msimu huu, katika mchezo wa raundi ya kwanza, Azam FC ilishinda ugenini kwa bao 1-0 lililofungwa na kiungo Tafadzwa Kutinyu, akimalizia kazi nzuri ya Mbaraka Yusuph.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amejipanga kuendeleza ushindi kwenye mechi ya tatu mfululizo ya ligi baada ya mechi mbili zilizopita kuzichapa Mwadui (1-0) na Biashara United kabla ya hapo ikitoka suluhu ya ugenini dhidi ya Ruvu Shooting.

Mabingwa hao wa ligi msimu wa 2013/2014, watamkosa beki wake wa kushoto, Bruce Kangwa, mwenye ruhusa maalumu akishughulikia matatizo ya kifamilia nchini kwao Zimbabwe, lakini hakuna shaka nafasi yake itazibwa na Hassan Mwasapili.

Hiyo itakuwa ni mechi ya 12 ya nyumbani ya Azam FC msimu huu kwenye ligi, hadi sasa ikiwa haijapoteza yoyote, ikishinda mara 10 na sare moja, iliyotoka na Lipuli (0-0), ikiwa ni rekodi bora ya nyumbani kuliko timu yoyote msimu huu.

Mara baada ya mchezo huo, Azam FC itakuwa na kibarua cha mechi tatu mfululizo za ugenini, ikianza na Lipuli Februari 11, kabla ya kuchuana na Tanzania Prisons Februari 14 huku ikihitimsha na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani Februari 19 mwaka huu.