MSIMU huu Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeamua kufanya kweli kwenye kila michuano inayoshiriki hadi sasa ikionekana kuwa na rekodi kabambe.

Mabingwa hao wameonekana kuwa na fomu nzuri msimu huu hadi sasa wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) ikiwa na pointi 47 ikizidiwa pointi sita na Yanga iliyokileleni kwa pointi 53.

Azam FC mbali na kufanya vema kwenye ligi, pia imekuwa na mwenendo bora kabisa katika michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) hadi sasa ikiwa imetinga raundi ya tano, ambayo inahusisha timu 16 bora.

Nyumbani haishikiki

Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, wamekuwa na rekodi bora kwenye uwanja wake huo msimu huu, hadi sasa ikiwa imecheza mechi 13 za mashindano mbalimbali (Ligi Kuu na Kombe la FA).

Wababe hao wamefanikiwa kushinda asilimia 99 za mechi zote ilizocheza hapo, ikishinda 12, mchezo mmoja ikitoka sare na ikiwa haijapoteza hata mmoja. Mechi pekee iliyotoka sare ni ile ya ligi dhidi ya Lipuli (0-0).

Mara ya mwisho Azam FC kufungwa ndani ya dakika 90, ilikuwa ni mwaka mmoja uliopita, dhidi ya Yanga Januari 27 mwaka jana, Shaaban Idd akiitanguliza mbele timu hiyo kabla ya Yanga kusawazisha na kushinda 2-1.

Mechi pekee iliyopoteza baada ya hapo ni ile dhidi ya Mtibwa Sugar, ikitolewa kwenye raundi ya 16 bora ya Kombe la FA kwa mikwaju ya penalti 9-8 kufuatia suluhu ndani ya dakika 90.

Ni mechi tisa tu za ligi ambazo Azam FC imecheza ugenini msimu huu, kati ya hizo imeshinda nne, sare nne na kupoteza mmoja ilipokipiga na Mtibwa Sugar (2-0), bado ikionekana si rekodi mbaya kwa mechi za ugenini.

Mataji wabeba 

Wakati msimu ukielekea kukamilika kwa raundi ya pili, hadi sasa Azam FC imeshaweka kibindoni mataji mawili kwa historia ya aina yake, ikilitwaa taji la Kagame kwa mara ya pili mfululizo Julai mwaka jana, ikiwa imelitetea baada ya kulibeba awali Agosti 2, 2015.

Mwaka huu ikaanza kwa mafanikio mengine, ikiandika rekodi ya kihistoria kwa kulitwaa jumla jumla Kombe la la Mapinduzi, ikiwa ndio timu ya kwanza kufanya hivyo baada ya kulitwaa taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo.

Aidha kwa Azam FC kubeba mataji hayo, sambamba na kuzoa medali za dhahabu na vikombe, pia imevuna kitita cha zaidi ya Sh. milioni 80, kwani bingwa wa Kagame huzawadiwa kitita cha Dola za Marekani 60,000 na kwa kutwaa Kombe la Mapinduzi ilipata Sh. milioni 15 kutoka kwa waandaji.

Washambuliaji wake wawili, waliweza kuandika rekodi ya michuano, Shaaban Idd, aliyetimkia CD Tenerife ya Hispania kabla ya mwezi huu kuhamishiwa CD Izarra kwa mkopo, aliibuka mfungaji bora wa Kagame kwa rekodi ya kihistoria ya mabao nane.

Akitoka kujiunga na kikosi hicho kwenye dirisha dogo, mshambuliaji Obrey Chirwa, aliyeifungia bao la ushindi Azam FC na kuiongoza kuichapa Simba 2-1 kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi, aliibuka mfungaji bora michuano hiyo kwa mabao matano aliyoweka kambani.

Hadi sasa Azam FC, ikiwa na kiu kubwa ya kurejea kwenye michuano ya Afrika msimu ujao, inaendelea vema kukabana koo kuwania mataji mawili iliyobakiza, Ligi Kuu na Kombe la FA.

Ni jambo la kusubiri katika miezi minne iliyobaki ya kuhitimisha msimu huu, kama Azam FC inaweza kuendeleza moto wa kutwaa mataji? Kazi ambayo inaweza kuitimiza kama ikijipanga vema kwani kitakwimu ipo vizuri na ina kikosi bora kabisa kinachoweza kumalizia vema mfupa huo uliobakia.