KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetinga hatua ya 16 ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya kuichapa Pamba mabao 2-0 mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Azam FC kwa kutinga hatua hiyo, sasa kwenye raundi ya tano itakutana Rhino Rangers ya Tabora, mchezo utakaofanyika tena kwenye dimba hilo kati ya Februari 22 hadi 25 mwaka huu.

Rangers inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL), imefuzu hatua hiyo baada ya kuitoa Stand United jana, ikishinda nyumbani kwa ushindi wa bao 1-0.

Mabingwa hao, walifanikiwa kutawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa na iliwachukua dakika 18 kupata bao la uongozi, lililofungwa na winga Ramadhan Singano ‘Messi’, akimalizia krosi iliyopigwa na beki wa kushoto, Nickolas Wadada.

Singano, aliihakikishia ushindi Azam FC, baada ya kurejea tena wavuni akiipatia bao la pili timu yake , akimalizia pasi ya mpenyezo aliyopigiwa na kiungo Mudathir Yahya.

Winga huyo kwa kufunga mabao hayo, sasa anaandika rekodi ya kufunga mabao matatu ndani ya mechi mbili mfululizo alizocheza, jingine akifunga wakati Azam FC ikiichapa Biashara United mabao 2-1.

Wababe hao kutoka viunga vya Azam Complex, wamejipanga vema kuweza kutwaa taji la michuano hiyo, ili kurejea kwenye michuano ya kimataifa, kwani bingwa ataweza kuiwakilisha Tanzania Bara katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kurejea mazoezini keshokutwa Jumatano kujiandaa na mechi ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) itakayocheza dhidi ya Alliance Februari 6 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC:

Mwadini Ally, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Agrey Moris (C), Yakubu Mohammed, Stephan Kingue/Salmin Hoza dk 65, Obrey Chirwa, Mudathir Yahya/Danny Lyanga dk 70, Donald Ngoma/Joseph Mahundi dk 65, Salum Abubakar, Ramadhan Singano