BAADA ya kuichapa Biashara United ya Musoma, kikosi cha Azam FC sasa kinahimishia nguvu yake kwenye mchezo wa raundi ya nne ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Pamba utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Jumatatu saa 1.00 usiku.

Azam FC imeingia raundi hiyo baada ya kuitoa Madini ya Arusha kwenye hatua iliyopita ikiichapa mabao 2-0, yaliyofungwa na winga Enock Atta na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Yahya Zayd, aliyetimkia Ismaily ya Misri huku Pamba inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ikiifunga Mtwivila City ya Iringa 4-1.

Mabingwa hao mara tatu mfululizo wa Kombe la Mapinduzi, wamejinasibu kuuchukulia kwa uzito mchezo huo huku Kocha Hans Van Der Pluijm, akidokeza kuwa wanatakiwa kujiandaa vema kimwili, kisaikolojia na kiakili kutokana na umuhimu wa mchezo huo.

“Ni vigumu daima kucheza dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza kwa sababu hawana cha kupoteza, tunapaswa kujiandaa kimwili, kisaikolojia na kiakili vizuri sana kwa mechi hii ya Kombe la FA,” alisema Pluijm wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz juzi.

Ushindi wowote kwa Azam FC kwenye mchezo huo, utaifanya kusonga mbele kwa hatua ya tano, ambayo itahusisha timu 16 bora, na hivyo kuisogelea karibu zaidi fainali ya michuano hiyo, kama ambavyo ilivyojiwekea malengo ya kufika hatua hiyo na kutwaa taji hilo msimu huu.

Aidha kwa Azam FC kutwaa taji hilo, basi itakuwa imekata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, mafanikio yatakayoifanya kuondoa rekodi mbaya ya kutofuzu michuano ya Afrika kwa misimu miwili mfululizo toka iliposhiriki mara ya mwisho mwaka juzi.

Fainali ya mwisho ya Azam FC kuingia kwenye michuano hiyo ilikuwa ni msimu 2015/2016, ilipokutana na Yanga na kufungwa mabao 3-1, bao la matajiri hao likiwekwa kimiani na mshambuliaji wa zamani, Didier Kavumbagu.