KOCHA Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amekiri ugumu walioupata kwenye mchezo dhidi ya Biashara United huku akidai wachezaji wake walipambana na kutambua wanapaswa kushinda.

Azam FC iliweza kutoka nyuma na hatimaye kuibuka na ushindi wa 2-1 katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika jana usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, mabao yaliyofungwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Ramadhan Singano ‘Messi’.

Pluijm ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa amefurahishwa sana na mchezo mzuri wa wachezaji wake, ari ya kupambana waliyoionyesha mwanzo hadi mwisho wa mtanange huo.

“Ilikuwa ni mechi ngumu sana, ikiwa upo nyuma bao 1-0 dakika ya pili ya mchezo unapaswa kupambana dhidi ya mpinzani aliyerudi nyuma kuzuia kwenye nusu yao, baada ya kufunga walikuwa wakicheza wachezaji tisa hadi 10 nyuma ya mpira.

“Ilikuwa ni ngumu sana kupata nafasi ya kuingia kwenye eneo lao, hata timu kubwa za Ulaya zingepata shida kutengeneza nafasi, lakini bado tuliweza kutengeneza nafasi kwa bahati mbaya tulishindwa kuzitumia,” alisema.

Akiwasifia wachezaji wake, alisema: “Bao la kusawazisha lilikuja kwenye wakati sahihi dakika moja baada ya mapumziko, ninawasifu vijana kwa ari kubwa na moyo wa kupambana walioonyesha hadi mwisho, walicheza kwa kuamini kuwa tunapaswa kushinda.”

Mara baada ya mchezo huo, kesho Jumapili kikosi cha Azam FC kitafanya mazoezi kujiandaa na mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Pamba ya mkoani Mwanza, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex keshokutwa Jumatatu saa 1.00 usiku.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha huyo raia wa Uholanzi, alisema kuwa hawataidharau Pamba badala yake wanatakiwa kucheza mchezo huo kama wanacheza fainali kutokana na umuhimu wa michuano hiyo.

“Tunapaswa kurejea kwenye hali yetu vizuri mara baada ya mchezo wa jana na kucheza kwa ari ile ile tuliyoionyesha usiku wa jana, hatuwezi kuidharau Pamba, tunapaswa kuanza mchezo kama tunacheza fainali,” alisema.

Pluijm alingeza kuwa; “Ni vigumu daima kucheza dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza kwa sababu hawana cha kupoteza, tunapaswa kujiandaa kimwili, kisaikolojia na kiakili vizuri sana kwa mechi hii ya Kombe la FA.”

Mabingwa hao wa michuano ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) msimu huu wakitwaa mara mbili mfululizo, na mara tatu mfululizo ikitwaa Kombe la Mapinduzi mwaka huu, kwa ushindi dhidi ya Biashara imefikisha pointi 47 katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikizidiwa pointi sita na Yanga iliyokileleni kwa pointi 53.