WACHEZAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na winga Enock Atta wameng’ara baaday kutwaa za mwezi za timu hiyo mwezi Novemba na Desemba mwaka jana.

Tuzo hizo zinakujia kwa udhamini wa vinywaji safi kutoka Kampuni ya Bakhresa Food Products, Juisi safi za African Fruti na Maji safi ya Uhai Drinking Water, ambapo wachezaji hao watapata tuzo maalum za ushindi.

Sure Boy alikuwa kwenye ubora mkubwa akifanya vema kwenye eneo la kiungo na kuiongoza Azam FC kuzoa pointi sita mwezi Novemba, ikishinda ugenini kwa kuichapa Kagera Sugar (1-0) na ushindi mwingine nyumbani dhidi ya Ruvu Shooting (2-1).

Ubora wake ulimfanya kurejeshwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ chini ya Kocha Mkuu, Emmanuel Amunike, kilichokuwa kikijiandaa na mechi dhidi ya Lesotho ugenini kwenye kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwaka huu nchini Misri.

Atta ambaye ameonekana kuwa moto msimu huu, amepata tuzo hiyo ya mwezi Desemba, baada ya kufunga mabao mawili na kutoa pasi mbili za mwisho, alifunga bao moja wakati Azam FC kiichapa Stand United 3-1 na jingine alifunga kwenye Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) walipilaza Madini 2-0.

Kwa upande wa timu ya vijana ya Azam FC (Azam U-20), tuzo ya mwezi Novemba imeenda kwa beki wa kushoto Abdallah Madirisha na ile ya Desemba imechukuliwa na beki aliyepandishwa timu kubwa, Samwel Onditi.

Onditi atakumbukwa kwa kiwango kizuri alichokionyesha kwenye timu kubwa akicheza kama beki wa kulia, wakati Azam FC ikiichapa Mwadui bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).