KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeendeleza wimbi la ushindi kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) baada ya kuichapa Biashara United mabao 2-1.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kupunguza pengo la pointi baina yake na kinara Yanga mwenye pointi 53,kufikia pointi sita baada ya kufikisha jumla ya pointi 47.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kubwa, Biashara United ikianza kuiduwaza Azam FC kwa bao la mapema dakika ya pili lililofungwa kwa kichwa na Daniel Manyenye.

Azam FC ilijitahidi kutafuta bao la kusawazisha lakini Biashara ilionekana kucheza kwa kupoteza muda, wachezaji wake wakijidondosha mara kwa mara wakidai wameumia, jambo ambalo lilifanya kipa wa timu hiyo, Nurdin Balora, aonyeshwe kadi ya njano.

Licha ya majaribio kadhaa langoni mwa Biashara United, yaliyofanywa na kiungo Mudathir Yahya, mshambuliaji Obrey Chirwa na winga Ramadhan Singano ‘Messi’, lakini kipa wa timu hiyo alionekana kusimama vema kuokoa michomo yote na kufanya mpira kwenda mapumziko kwa uongozi wa wageni hao.

Kipindi cha pili, Azam FC ilianza kwa kasi ikitaka kupata bao la mapema, ambapo jitihada hizo zilifanikiwa dakika ya 46 kwa bao safi la kichwa lililofungwa na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, aliyeunganishwa krosi safi ya Chirwa na kuisawazishia timu hiyo.

Hilo ni bao la tatu la Sure Boy, kwenye msimu huu wa ligi, mengine alifunga wakati Azam FC ikitoa sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Mwadui na jingine akitupia walipoichapa Mbao 4-0.

Mabingwa hao mara tatu mfululizo wa Kombe la Mapinduzi na mara mbili mfululizo wa Kombe la Kagame, waliendeleza kasi yao, ambayo ilizaa matunda kwa kupata bao la ushindi dakika ya 62 lililowekwa kimiani na Singano, aliyemalizia pasi safi ya Sure Boy.

Mara baada ya ushindi huo, kikosi cha Azam FC kinaendelea kusalia kambini, ambapo kitarejea mazoezini Jumapili jioni kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Pamba ya Mwanza unaotarajia kufanyika Uwanja wa Azam Complex Jumatatu ijayo saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Stephan Kingue, Obrey Chirwa, Mudathir Yahya, Donald Ngoma/Danny Lyanga dk 83, Salum Abubakar, Ramadhan Singano/Joseph Mahundi dk 71