WAKATI zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya Azam FC kumenyana na Biashara United, kikosi hicho kimejinasibu kuendelea kupata matokeo mazuri ili kufikia malengo yake.

Mabingwa hao wa makombe mawili msimu huu baada ya kufanikiwa kutetea Kombe la Kagame na Mapinduzi Cup, wamekuwa kwenye mwenendo mzuri msimu huu hadi sasa ikishika nafasi ya pili kwenye za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) ikiwa na pointi 44.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Nahodha wa Azam FC, Agrey Moris, amesema kuwa wanajua mchezo utakuwa mgumu lakini watajipanga vema kuweza kupata matokeo.

“Biashara ni timu nzuri ukiangalia wamepata kocha mpya kwa vyovyote timu inayopata kocha mpya wachezaji wanakuwa wanajitolea mara mbili zaidi ya mwanzo ila kama sisi Azam siku zote tunajipanga kuhakikisha tunapata matokeo kwenye michezo yetu.

“Kwa sababu hii ni ligi ni safari ndefu bila kushinda mechi inayokuja mbele huwezi ukafikia lengo, tumejipanga vizuri wachezaji wote wako vizuri tutahakikisha tunapata matokeo kwenye mchezo huo,” alisema mchezaji huyo wa muda mrefu wa Azam FC.

Kihistoria timu hizo zimekutana mara moja tu kwenye ligi, tokea Biashara ipande kucheza Ligi Kuu msimu huu, ambapo mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Karume, mjini Musoma uliisha kwa suluhu.

Katika kuinusuru timu hiyo kutoshuka daraja, Biashara kwa sasa inaye kocha mpya, Amri Said, aliyejiuzulu kuifundisha Mbao mwishoni mwa mwaka jana.