BAO pekee lililofungwa na mshambuliaji Donald Ngoma, limeiongoza Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kuzoa pointi tatu muhimu dhidi ya Mwadui.

Ushindi huo unawafanya mabingwa hao mara tatu mfululizo wa Kombe la Mapinduzi, kufikisha pointi 44 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) ikizidiwa pointi tisa na vinara Yanga iliyokuwa nazo 53, huku ikiwa pia na mchezo mmoja mkononi.

Mabingwa hao waliingia kwenye mchezo huo wakiwakosa takribani nyota wake 10 kwa sababu mbalimbali, nahodha Agrey Moris, Nickolas Wadada, ambao wamekusanya kadi tatu za njano, David Mwantika, Abdallah Kheri, Daniel Amoah, Tafadzwa Kutinyu, Frank Domayo, Joseph Kimwaga, Peter Paul, wote wakiwa majeruhi huku winga Enock Atta, akiwa tayari amejiunga na timu ya Taifa ya Ghana ‘Ghana U-20’.

Benchi la ufundi la Azam FC, lililazimika kuwajumuisha kwenye kikosi kilichoanza wachezaji watatu kutoka timu ya vijana ‘Azam U-20’, beki wa kati Lusajo Mwaikenda, beki wa kulia Samweli Onditi na benchini alikuwepo beki mwingine Samweli Ndumieni.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, ulikuwa ni wa ushindani mkubwa kwa pande zote mbili na haikuwa kazi rahisi kwa mabingwa hao kupata bao hilo.

Azam FC ilianza mchezo kwa kasi na kukosa takribani nafasi tatu za wazi za kufunga mabao dakika 30 za mwanzo, mbili zikipotezwa na kiungo Mudathir Yahya.

Mabadiliko ya kuingia mshambuliaji Donald Ngoma, mwanzoni mwa kipindi cha pili akichukua nafasi ya Mudathir, yaliongeza kasi ya kwenye eneo la ushambuliaji hali iliyowafanya wachezaji wa Mwadui kujiangusha mara kwa mara ili kupoteza muda.

Dakika ya 69, mpira mrefu uliopigwa na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, uliweza kutumiwa vema na Ngoma, ambaye alimzidi mbio kipa wa Mwadui na kuunganisha mpira uliokwenda nyavuni na kuihakikishia ushindi Azam FC iliyosogea kwa pointi kuelekea kileleni mwa msimamo wa ligi.

Aidha matokeo hayo yameiweka kwenye mstari wa ushindi Azam FC, ambayo ilikosa matokeo ya aina hiyo kwenye mechi mbili zilizopita za ligi ugenini, awali ikipoteza mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kabla ya kutoka suluhu na Ruvu Shooting Jumatano iliyopita.

Mara baada ya mchezo huo, Azam FC inahamishia makali yake kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) ambapo imepangwa kucheza na Pamba kati ya Januari 25 hadi 28 mwaka huu, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Samweli Onditi, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed (C), Lusajo Mwaikenda, Stephan Kingue, Joseph Mahundi, Mudathir Yahya/Donald Ngoma dk 46, Obrey Chirwa/Danny Lyanga dk 81, Salum Abubakar, Ramadhan Singano/Idd Kipagwile dk 70