BAADA ya kucheza mechi mbili mfululizo za ugenini kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inarejea nyumbani Azam Complex kukipiga dhidi ya Mwadui kesho Jumamosi saa 1.00 usiku.

Azam FC imefanikiwa kuondoka na pointi moja katika hizo mbili, ikipoteza kwa mara ya kwanza msimu huu dhidi ya Mtibwa Sugar (2-0) na mchezo uliopita ikitoka suluhu na Ruvu Shooting, hadi sasa ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 41 ilizojikusanyia.

Mabingwa hao wamekuwa na mwendelezo wa mazoezi, wakianza jana usiku yote ni katika kujipanga vilivyo kuelekea mchezo huo, ambao ni muhimu kwa timu hiyo kupata matokeo ya ushindi.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amesema kuwa licha ya kuwakosa wachezaji wake kadhaa wa kikosi cha kwanza, amedai ni mchezo wanaotakiwa lazima kushinda.

“Mchezo huo utakuwa mgumu, Mwadui ni timu nzuri nayo, pia unajua kila timu inapocheza na Azam inajitahidi kucheza zaidi ya kiwango chao halisi, kuliko wanapocheza na timu nyingine, kiukweli ni mechi ambayo tunatakiwa kushinda,” alisema.

Timu hizo zilipokutana raundi ya kwanza kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, zilitoka sare ya bao 1-1, bao la Azam FC likiwekwa kimiani na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kabla ya Charles Ilanfya kusawazisha.

Mara ya mwisho kukutana kwenye Uwanja wa Azam Complex, msimu uliopita Azam FC ilishinda bao 1-0 lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Yahya Zayd, aliyetimkia Ismaily ya Misri, ambaye alitumia uzembe wa kipa Anold Masawe.

Kihistoria kwenye mechi za ligi, Azam FC imekutana mara saba na Mwadui, ikiwa imeshinda jumla ya mechi tano na kutoka sare mbili, zote ikipata ugenini kwenye dimba la Mwadui Complex.