KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeondoka na pointi moja kwenye Uwanja wa Mabatini baada ya kutoka suluhu na wenyeji wao, Ruvu Shooting, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika leo Jumatano jioni.

Sare hiyo inaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 41 katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa tofauti ya pointi 12 na vinara Yanga wenye pointi 53, lakini matajiri hao wakiwa na mchezo mmoja mkononi.

Kikosi cha Azam FC kilijitahidi kusaka ushindi kwenye mchezo huo, lakini kwa kiasi kikubwa hali mbaya ya uwanja ilipelekea pambano hilo kutokuwa na ladha yoyote, jambo ambalo limeziathiri timu zote mbili.

Azam FC ilipoteza nafasi kadhaa kipindi cha kwanza, ya kwanza ilimhusisha winga Joseph Mahundi, ambaye alikaribia kuiandikia bao la uongozi timu hiyo baada ya kupiga shuti zuri ndani ya eneo la 18 lakini kipa wa Ruvu Shooting alipangua mpira na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Kuelekea mwishoni mwa mchezo huo, Obrey Chirwa, alipiga krosi safi kwa Donald Ngoma, ambaye alipiga kichwa cha kudunda chini na mpira kuelekea golini lakini kipa wa Ruvu aliondoa mpira kwenye mstari na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Wachezaji wa Azam FC, nahodha Agrey Moris na Nickolas Wadada, waliweza kuonyeshwa kadi za njano kwenye mchezo huo, zinazowafanya kuukosa mchezo ujao dhidi ya Mwadui kutokana na kukusanya kadi tatu za njano.

Azam FC inatarajia kushuka tena dimbani Jumamosi hii kukipiga na Mwadui, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kuanzia saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora/Mwadini Ally dk 46, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Stephan Kingue, Joseph Mahundi/Idd Kipagwile dk 85, Mudathir Yahya/Donald Ngoma dk 70, Obrey Chirwa, Salum Abubakar, Ramadhan Singano