BAADA ya kutwaa taji la Kombe la Mapinduzi mwishoni wa wiki iliyopita, kikosi cha Azam FC kinatarajia kushuka dimbani kuvaana na Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi Pwani kesho Jumatano saa 10.00 jioni.

Azam FC iliyoonyesha umwamba kwenye michuano ya Mapinduzi, wachezaji wake wataingia katika mchezo huo, wakiwa na morali ya hali juu kutokana na kutwaa taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo na kulibeba jumla jumla.

Mabingwa hao waliweza kuwatambia Ruvu kwenye mchezo wa raundi ya kwanza, baada ya kuichapa kwa mabao 2-1, yaliyofungwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ na Tafadzwa Kutinyu, huku lile la Ruvu likiwekwa kimiani na Said Dilunga.

Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amesema kuwa wanaingia kwenye mchezo huo wakihitaji ushindi licha ya kukiri kukabiliana na changamoto kubwa ya ubovu wa Uwanja wa Mabatini.

“Baada ya kurejea kutoka Kombe la Mapinduzi tukiwa mabingwa, tumewaambia tayari wachezaji kuweka nyuma yote na kuweka umakini kwenye mechi ya kesho dhidi ya Ruvu Shooting, na kila mmoja anajua jinsi wanavyocheza wakati wanacheza nyumbani, wanacheza kwa kukamia sana.

“Pia uwanja si mzuri, tunapaswa kujiandaa hasa kisaikolojia na kimwili vizuri sana, wao wanaujua vizuri sana uwanja, wanafanya mazoezi na kufanya kazi pale, tunatakiwa kubadili malengo yetu na kutumia staili nyingine ya uchezaji, kupitia kile tulichojifunza kwenye mazoezi leo,” alisema.

Mabingwa hao wa ligi msimu wa 2013/2014, wanaingia kwenye mchezo huo wakiwakosa wachezaji wake kadhaa ambao ni wagonjwa, beki David Mwantika, kiungo Tafadzwa Kutinyu na winga Enock Atta, anayetarajia kuondoka nchini kesho Jumatano kuelekea nchini kwao Ghana.

Atta aliyekuwa kwenye kiwango bora kabisa msimu huu, anaelekea huko kujiunga na timu ya Taifa chini ya umri wa miaka 20 ‘Black Sattelite’ inayojiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchini Niger, kuanzia Februari 2 hadi 17 mwaka huu.

Hadi sasa kwenye msimamo wa ligi, Azam FC inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 40 nyuma ya Yanga iliyo kileleni kwa pointi 50 lakini ikizidiwa mechi mbili.     

Rekodi (H2H)

Kihistoria timu hizo zimekutana mara 15, ambapo Azam FC imeshinda mara tisa, ikifungwa mara moja na mechi tano zilizobakia zikiisha kwa sare.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye Uwanja wa Mabatini, Azam FC ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0, lakini kicheza pungufu ya mchezaji mmoja kipindi cha pili baada ya mwamuzi wa mchezo huo, Shomari Lawi, kumuonyesha kadi ya pili ya njano na nyekundu nahodha Agrey Moris.