WINGA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Enock Atta, ni miongoni mwa wachezaji 25 wa timu ya Taifa ya vijana ya Ghana chini ya umri wa miaka 20 ‘Black Satellites’ walioitwa kwa ajili ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana (AFCON U-20).

Fainali hizo zinatarajia kufanyika nchini Niger katika miji ya Niamey na Maradi kuanzia Februari 2 hadi 17 mwaka huu, Ghana ikiwa Kundi B sambamba na Senegal, Mali na Burkina Faso.

Hii ni mara ya pili kwa Atta kupokea mwaliko huo, awali ilikuwa ni Agosti mwaka jana alipokwenda kucheza mechi mbili za kufuzu fainali hizo dhidi ya Benin, baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 4-2, ikishinda nyumbani 3-1 na kutoka sare ya 1-1 jijini Cotonou, Benin.

Akizungumzia uteuzi wake kushiriki michuano hiyo chini ya Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Jimmy Cobblah, Atta ameuambia mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz  kuwa amefurahishwa sana huku akidai malengo yake ni kupambana kuisaidia timu hiyo kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia la vijana na kushinda taji hilo.

“Unajua ukiwa mchezaji na ukaitwa timu ya Taifa ya nchi yako basi unajisikia heshima kubwa, nikiwa kama sehemu ya kikosi nimefurahishwa sana na uteuzi huo, malengo yangu hivi sasa na wachezaji wenzangu ni kupambana na kuhakikisha tunafuzu kwa fainali za Kombe la Dunia na kubeba taji hilo,” alisema.

Atta alisema ataitumia fursa hiyo kucheza kwa kiwango cha juu ili kujitangaza na kuliweka jina la Azam FC juu zaidi kupitia mafanikio yake, kwa kuwa ndio timu anayochezea iliyomfanya hadi kupata uteuzi huo.

Winga huyo anayetarajia kuondoka nchini keshokutwa Jumatano kujiunga kambini na wenzake, amekuwa na kiwango bora msimu huu hadi sasa.