KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeandika rekodi mpya kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, ya kulitwaa taji hilo mara tatu mfululizo baada ya kuichapa Simba mabao 2-1 kwenye mchezo wa fainali uliofanyika Uwanja wa Gombani, Pemba.

Azam FC kulitwaa taji hilo, hiyo inamaanisha kuwa inakabidhiwa moja kwa moja kikombe cha michuano hiyo kutokana na sheria za waandaaji kueleza kuwa timu yote itakayobeba mara tatu mfululizo basi kombe litakuwa lake.

Mabingwa hao waliofanikiwa kutawala mchezo huo hasa kipindi cha pili, waliweza kujipatia bao la uongozi dakika ya 44 lililofungwa na kiungo Mudathir Yahya, kwa shuti kali nje kidogo ya eneo la 18 akimalizia kazi nzuri ya winga Enock Atta.

Bao hilo lilidumu hadi kumalizika kwa kipindi cha kwanza, ambapo kipindi cha pili dakika ya 63, Simba ilisawazisha kupitia kwa beki wake, Yusuf Mlipili, aliyeunganisha kwa kichwa kona iliyochongwa na Shiza Kichuya.

Mshambuliaji Obrey Chirwa, aliyeibuka mfungaji bora wa michuano hiyo, aliihakikishia ubingwa Azam FC baada ya kuipatia bao la pili dakika ya 72, likiwa ni bao lake la tano, akimalizia krosi ya beki wa kushoto, Nickolas Wadada.

Hilo linakuwa taji la tano la Azam FC kwenye michuano hiyo, ikiwa ndio timu iliyolibeba mara nyingi kuliko timu yoyote, ikilitwaa kwa mara ya kwanza mwaka 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Stephan Kingue, Tafadzwa Kutinyu/Ramadhan Singano dk 24, Mudathir Yahya, Obrey Chirwa/Donald Ngoma dk 88, Salum Abubakar, Enock Atta