ZIMEBAKI saa kadhaa kabla ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kuvaana na Simba katika fainali ya Kombe la Mapinduzi itakayofanyika Uwanja wa Gombani, Pemba kesho Jumapili saa 9.30 jioni.

Wakati Azam FC ikitinga fainali baada ya kuichapa KMKM mabao 3-0, Simba yenyewe imeshinda kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 3-1 dhidi ya Malindi kufuatia dakika 90 kumalizika kwa suluhu.

Mchezo huo unakumbushia fainali ya mwaka 2017, Azam FC ilipoifunga Simba bao 1-0, bao lililofungwa na nahodha wa zamani wa timu hiyo, Himid Mao ‘Ninja’, kwa shuti la mbali lililomshinda aliyekuwa kipa wa Simba, Daniel Agyei.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikisaka taji la tano la michuano hiyo, na ubingwa wa tatu mfululizo, utakaoifanya kuandika rekodi mpya ya kuwa timu pekee kuwahi kufanya hivyo.

Kila ikiingia fainali, Azam FC mara zote imeweza kufanikiwa kutwaa taji hilo, ambapo kihistoria imelitwaa mwaka 2012, 2013, 2017, 2018.

Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amesema kuwa wachezaji wan ari kubwa huku akijinasibu ya kuwa anaamini kikosi chake kitaibuka na ubingwa.

“Timu ina ari nzuri, hatukucheza vizuri mechi ya kwanza tu mechi zilizofuatia tulicheza vema kwa kujiamini, tukiwa na mpira, bila mpira tumekuwa tukikaba vema, kama nilivyotangulia kusema unaposhiriki michuano na unataka kushinda taji, unatakiwa kukutana na wapinzani wagumu na unatakiwa kuwafunga, sisi tuko tayari kwa hilo,” alisema.

Mshambuliaji wa Azam FC, Obrey Chirwa, ataingia kwenye mchezo huo akitaka kuendeleza moto wake wa kufunga mabao hadi sasa akiwa ndiye kinara wa kupachika mabao kwenye michuano hiyo, akiwa amefunga manne.

Wanaomfuatia kwa upachikaji mabao kwa upande wa Azam FC, ni mshambuliaji Donald Ngoma, aliyetungua mawili, nahodha Agrey Moris, naye akiwa amefunga mawili hadi sasa, yote akifunga kwa staili ya kichwa.

Msafara wa Azam FC, unatarajia kuondoka Unguja, Zanzibar kesho Jumapili asubuhi kwa usafiri wa ndege tayari kuelekea Pemba kwa mchezo huo wa fainali, unaosubiriwa na mashabiki wengi wa soka.