KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetinga fainali ya tatu mfululizo ya michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa KMKM mabao 3-0, mchezo wa nusu fainali uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Azam FC hivi sasa inasubiria kujua mpinzani wake katika mechi ya fainali, ambaye huenda ikawa Simba au Malindi ambazo zitacheza nusu fainali ya pili saa 2.15 usiku.

Nahodha wa Azam FC, Agrey Moris, alianzisha safari ya timu hiyo fainali akifunga bao la kwanza dakika ya tisa, kwa kichwa akimalizia mpira wa kona uliochongwa na winga Enock Atta.

Hilo ni bao la pili kwa Moris kwenye michuano hiyo msimu huu, yote akifunga kwa staili moja ya kichwa, jingine akitupia wakati Azam FC ikiilaza Malindi 2-1, akimalizia kona iliyopigwa na Mudathir Yahya.

Kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, alizidi kuikata maini KMKM baada ya kufunga bao safi la pili akimalizia mpira wa krosi ya chini uliopigwa na beki wa kulia, Nickolas Wadada.

Dakika ya 81, mshambuliaji Obrey Chirwa, alidhihirisha kuwa anautaka ufungaji bora wa michuano hiyo baada ya kufunga bao lake la nne, likiwa ni la tatu kwa Azam FC, akihitimisha ushindi huo mnono kwa matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex.

Kwa kuingia hatua ya fainali, Azam FC inafukuzia taji la tatu mfululizo la michuano hiyo baada ya kulitwaa mara mbili mfululizo (2017, 2018).

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa/Hassan Mwasapili dk 76, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C)/Lusajo Mwaikenda dk 86, Stephan Kingue/Novatus dk 84, Joseph Mahundi/Donald Ngoma dk 46, Mudathir Yahya/Tafadzwa Kutinyu, Obrey Chirwa, Salum Abubakar, Enock Atta