KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, ipo kamili kukipiga na KMKM katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2019 utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar kesho Ijumaa saa 10.15 jioni.

Hii ni nusu fainali ya tatu mfululizo, Azam FC inaingia katika michuano ikiwa inalifukuzia taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo, na imeingia hatua hiyo baada ya kumaliza kinara wa Kundi B ikifikisha pointi 10.

Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amesema kuwa mchezo huo utakuwa ni mgumu kutokana na aina ya mpinzani wanayekutana naye huku akidai watajitahidi kuweza kupata matokeo ili kufuzu kwa fainali ya michuano hiyo.

“Itakuwa ni mechi ngumu kwa sababu KMKM imemaliza nafasi ya pili kwenye kundi jingine, timu zote zinazocheza nusu fainali nadhani zitakuwa ngumu kucheza nazo na kama unataka kuwa bingwa lazima uzifunge zote.

“Tunatakiwa kuonyesha nidhamu ya mchezo kama tulivyofanya kwenye mechi ya mwisho jana usiku, ni timu ambayo inatumia nguvu sana na inacheza mpira, nadhani tuna timu nzuri inayoweza kufanya lolote linalowezekana kushinda mechi hiyo,” alisema.

Mshambuliaji wa Azam FC, Obrey Chirwa, amezidi kuonyesha ubora wake kwenye michuano hiyo hadi sasa akiwa amepachika mabao matatu akiwa anafukuzia ufungaji bora huku Donald Ngoma, akiwa ametupia mawili.

Nusu fainali ya pili ya michuano hiyo itakayopigwa siku hiyo itakuwa kati ya Simba na Malindi, itakayoanza saa 2.15 usiku.

Endapo Azam FC italitwaa taji hilo kwa ya mara tatu mfululizo basi itakuwa imejimilikisha taji la michuano hiyo na kuandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kuwahi kufanya hivyo.

Fainali ya michuano hiyo, inatarajia kupigwa kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba Jumapili hii saa 9.30 Alasiri, na bingwa wa michuano hiyo atavuna kitita cha Sh. Milioni 15, kombe na medali za dhahabu, mshindi wa pili atapata Milioni 10 na mshindi wa tatu Milioni 5.