DROO ya raundi ya nne ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) imefanyika leo, Azam FC ikipangwa kucheza na Pamba ya jijini Mwanza, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kati ya Januari 25 na 28 mwaka huu.

Azam FC iliingia raundi hiyo baada ya kuifumua Madini ya Arusha mabao 2-0, yaliyofungwa na winga Enock Atta na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Yahya Zayd, aliyetimkia Ismaily ya Misri mwanzoni mwa wiki hii.

Pamba yenyewe inakutana na mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, ikitoka kuichapa Mtwivila City ya Iringa mabao 4-1 kwenye mchezo wa raundi iliyopita uliofanyika mjini Iringa.

Kikosi cha Azam FC kimejidhatiti vilivyo kuweza kutwaa taji hilo ili kurejea kwenye michuano ya kimataifa Novemba mwaka huu, ambapo kama kawaida bingwa katika fainali itakayofanyika kwenye Uwanja wa Ilulu, mjini Lindi atakata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika (Azam Sports Federation Cup).

Endapo Azam FC itafanikiwa kuichapa Pamba kwenye raundi ya tano (hatua ya 16 bora), imepangwa kucheza tena dimba la nyumbani dhidi ya mshindi wa mechi ya raundi hii kati ya Rhino Rangers ya Tabora na Stand United ya Shinyanga.

Mechi nyingine Raundi ya 4 (hatua ya 32 bora):  

Rhino Rangers v Stand United

KMC v Pan Africans

Kagera Sugar v Mbeya Kwanza

Polisi Tanzania v Lipuli FC

Yanga v Biashara United

Kitayosco v Coastal Union

Singida United v JKT Tanzania

Mtibwa Sugar v Majimaji

Mashujaa v Mbeya City

Friends Rangers v African Lyon

Might Elephant v Namungo

Alliance v La Familia

Dodoma FC v Transit Camp

Cosmopolitan v Dar City

Reha FC v Boma FC