KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetinga nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2019 ikiwa kinara wa Kundi B, baada ya kuichapa Malindi mabao 2-1, mchezo uliomalizika kwenye Uwanja wa Amaan leo Jumatano usiku.

Azam FC sasa itacheza na KMKM iliyoshika nafasi ya pili kwenye Kundi A katika nusu fainali ya kwanza ya michuano hiyo itakayofanyika keshokutwa Ijumaa saa 10.15 jioni huku ikifuatiwa na nusu fainali ya pili kati ya Simba na Malindi itakayoanza saa 2.15 usiku siku hiyo.

Haikuwa kazi rahisi kwa Azam FC kumaliza ikiwa kinara wa kundi hilo kwani ililazimika kupambana vilivyo kuichapa Malindi, ambayo ilionekana kuonyesha upinzani wa kweli muda wote wa mchezo huo.

Mabingwa hao watetezi wa michuano hiyo wanaolisaka taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo, walianza kuziona nyavu za Malindi dakika ya 26 kwa bao safi la kichwa lililofungwa na nahodha, Agrey Moris, aliyeunganisha kona safi iliyochongwa na kiungo, Mudathir Yahya.

Bao hilo lilidumu hadi kumalizika kwa kipindi cha kwanza, ambapo mabadiliko yaliyofanywa kipindi cha pili na benchi la ufundi la Azam FC la kumuingiza mshambuliaji Donald Ngoma na kutoka Stephan Kingue, yaliongeza uhai kwenye eneo la ushambuliaji la timu hiyo.

Dakika ya 76, Ngoma alizidi kuihakikishia ushindi Azam FC baada ya kuifungia bao la pili akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Malindi, Ahmed Suleiman, kufuatia kupigiwa shuti kali la chini na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Malindi iliweza kujitutumua na kufanikiwa kupata bao la kufuatia machozi dakika ya 87 lililofungwa kwa shuti kali nje ya eneo la 18 na Abdulswamad Kassim.

Kikosi cha Azam FC kinafunga hatua ya makundi kikiwa kimemaliza kwa pointi 10, baada ya kushinda mechi tatu, ikichapa Yanga (3-0), KVZ (2-1), Malindi (2-1) na kutoka sare moja dhidi ya Jamhuri (1-1).

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada/Lusajo Mwaikenda dk 84, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C)/David Mwantika dk 84, Stephan Kingue/Donald Ngoma dk 59, Joseph Mahundi/Ramadhan Singano dk 59, Mudathir Yahya, Obrey Chirwa, Salum Abubakar, Enock Atta/Danny Lyanga dk 75