UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, unayofuraha kubwa kuthibitisha kufikia makubaliano na klabu ya Ismaily ya nchini Misri juu ya mauzo ya mshambuliaji chipukizi, Yahya Zayd.

Zayd, 20, yupo nchini Misri tayari hivi sasa kwa vigogo hao wa soka walioingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu, ambapo ameshamaliza taratibu zote za kimkataba baada ya awali kufuzu vipimo vya afya.

Ismaily imemsajili Zayd baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu na kuridhishwa na uwezo wake akiwa ni mchezaji ambaye anachipukia aliyekulia kwenye malezi ya soka Azam Academy na kupandishwa timu kubwa ya Azam FC msimu uliopita (2017-2018).

Licha ya kumuuza moja kwa moja Zayd, Azam FC itazidi kunufaika zaidi kiuchumi endapo Ismaily itamuuza mshambuliaji kwenda timu nyingine, ambapo klabu itapata mgawo wa asilimia 10 wa mauzo ya mchezaji huyo.

Mshambuliaji huyo mwenye uwezo wa kufunga na kutoa pasi za mabao, aliyekuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa ya Azam FC, alifanikiwa kucheza msimu mmoja kwa mkopo (2016-2017) katika kikosi cha Ashanti United inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Azam FC tunafuraha kubwa na kujivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya wachezaji vijana katika kutimiza ndoto zao za kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, ambapo Zayd anaongeza orodha ya wachezaji na kufikia wanne ambao wamepelekwa kucheza soka nje ya nchi na timu hiyo, wote wakiwa wamelelewa na Azam Academy.

Wachezaji wengine ni Farid Mussa, Shaaban Idd (wanaokipiga CD Tenerife ya Hispania) na nahodha wetu wa zamani, Himid Mao ‘Ninja’, ambaye naye anakipiga Petrojet ya nchini Misri aliyojiunga nayo Juni mwaka jana, ambapo tokea ajiunge nayo amekuwa mchezaji tegemeo wa kikosi hicho wiki iliyopita akifunga mabao mawili yaliyiongoza timu yake kutinga nusu fainali ya Kombe la Egypt ikiitungua ENPPI 2-1.

Uongozi wa Azam FC hivi sasa, umejiwekea malengo ya kuhakikisha inafanikisha zoezi la wachezaji wetu kucheza soka la kulipwa nje ya mipaka ya Tanzania, ambapo kila tutakapopokea ofa nzuri kwa maendeleo ya mchezaji wetu, hatutasita kuikubali, na tunaamini kupitia hilo klabu yetu itanufaika kujitangaza na kukua kiuchumi, pia itakuwa ni faida kwa mchezaji na Taifa kiujumla.

Zayd anaondoka akiwa amefunga jumla ya mabao sita msimu huu, matano akifunga Ligi Kuu na moja kwenye Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) huku akitoa pasi mbili za mwisho za mabao.

Azam FC tunamtakia kila la kheri Zayd katika maisha yake mapya ya soka kwenye klabu yake mpya, tunaamini kwa kipaji alichokuwa nacho atazidi kufika mbali na kuendelea kuitangaza klabu yetu.