KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetanguliza mguu mmoja kufuzu nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa KVZ mabao 2-1 jioni ya leo.

Azam FC imeibuka na ushindi huo na kufikisha jumla ya pointi saba ikiwa kileleni mwa Kundi B la michuano hiyo, ambalo linaonekana kuwa kundi gumu zaidi kwenye michuano hiyo kutokana na timu zote kukaribiana pointi.

Kikosi cha Azam FC kinahitaji ushindi wowote kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Malindi utakaofanyika keshokutwa Jumatano ili kuweza kufuzu kwa nusu fainali ya michuano hiyo.

KVZ ilianza kwa kushtua baada ya kutangulia kufunga bao la mapema dakika ya 16 lililofungwa na Amour Bakari, aliyemfanyia madhambi nahodha wa Azam FC, Agrey Moris kabla ya kufunga bao hilo.

Azam FC ililazimika isubiri hadi kipindi cha pili kuweza kupindua matokeo, hasa baada ya kuingia mshambuliaji Donald Ngoma, aliyeongeza kasi ya mashambulizi akishirikiana vema na Obrey Chirwa.

Dakika ya 75, Ngoma aliisawazishia Azam FC akifunga bao kwa shuti lililomshinda kipa wa KVZ, Yakubu Bakari na mpira kujaa wavuni, akitumia pasi ya Chirwa aliyepambana na mabeki kabla ya kupenyeza pande hilo.

Wakati watu wakidhani matokeo yangebakia hivyo hivyo, kona iliyochongwa na winga Ramadhan Singano ‘Messi’, dakika ya 90 ilimkuta Ngoma aliyemsetia kwa kichwa Chirwa, ambaye aliipatia Azam FC bao la pili kwa kichwa safi.

Hilo ni bao la tatu kwa Chirwa kwenye michuano hiyo, mawili alifunga kwenye mchezo uliopita wakati Azam FC ikiiadhibu Yanga mabao 3-0.

Kikosi Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Stephan Kingue, Idd Kipagwile/Danny Lyanga dk 46, Mudathir Yahya/Donald Ngoma dk 69, Obrey Chirwa, Salum Abubakar, Enock Atta/Ramadhan Singano dk 86