KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanya kweli baada ya kuichapa Yanga mabao 3-0 kwenye mchezo wa michuano ya Kombe la Mapinduzi uliomalizika leo Jumamosi usiku.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kupanda kileleni mwa msimamo wa Kundi B ikiwa na pointi nne sawa na Malindi lakini matajiri hao wakiwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga.

Azam FC ilianza vyema mchezo huo, dakika ya kwanza tu mshambuliaji Obrey Chirwa, alikosa nafasi ya wazi baada ya kupokea pasi safi ya Enock Atta na kupiga shuti lililodakwa na kipa wa Yanga, Ibrahim Hamid.

Chirwa alirekebisha makosa yake dakika ya 33 na akiipatia Azam FC bao la uongozi akimalizia pande safi la kiungo mshambuliaji, Tafadzwa Kutinyu.

Winga Enock Atta, aliyekuwa akisheherekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa leo, aliimaliza siku yake vema kwa kuipatia bao la pili Azam FC dakika ya 44 kwa mpira wa moja kwa moja adhabu ndogo, iliyotokana na Kutinyu kufanyiwa madhambi nje kidogo ya eneo la 18.

Kipindi cha pili Azam FC iliendelea kulisakama lango la Yanga, ambapo ilifanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 60 lililofungwa na Chirwa, ambaye alikuwa akiiadhibu kwa mara ya pili timu yake hiyo ya zamani.

Huo ni ushindi mnono wa tatu kwa Azam FC kwenye michuano hiyo dhidi ya Yanga, mwaka 2012 iliichapa mabao 3-1 huku pia ikiwa na rekodi ya kuinyuka mabao 4-0, ambapo mara zote ilipopata ushindi iliweza kutwaa taji la michuano hiyo.

Azam FC imebakiza mechi mbili kuhitimisha hatua ya makundi, ambapo Jumatatu ijayo inatarajia kukipiga na vinara wa Ligi Kuu Zanzibar, KVZ na kuhitimisha hatua ya makundi kwa kukipiga na Malindi Jumatano ijayo.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Stephan Kingue, Joseph Mahundi/Ramadhan Singano dk 79, Mudathir Yahya, Obrey Chirwa/Donald Ngoma dk 79, Tafadzwa Kutinyu, Enock Atta/Idd Kipagwile dk 85