KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa na shughuli pevu kwenye patashika ya michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2019, itakaposhuka dimbani kuvaana na Yanga, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar kesho Jumamosi saa 2.15 usiku.

Azam FC itaingia uwanjani ikitaka kurekebisha makosa ya mchezo wa kwanza iliocheza juzi ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Pemba, ambapo itakuwa ikisaka ushindi muhimu ili kujiweka kileleni mwa msimamo wa Kundi B.

Wachezaji wote wa Azam FC wapo kwenye hali nzuri kuelekea mchezo huo, isipokuwa wawili ambao ni majeruhi viungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Tafadzwa Kutinyu, ambao wanatarajia kuikosa mechi hiyo.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amesema kuwa watafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huo.

“Kwa bahati mbaya tuna majeruhi wawili Sure Boy, Kutinyu, tumeendelea kufanya kazi kwa bidii, tunawajenga wachezaji kiakili hatukuanza vema michuano kama tulivyokuwa tumepanga, tumejipanga kurejea tena vizuri, nimewaangalia Yanga wakicheza tutahakikisha tunafanya kila liwezekanalo kupata ushindi,” alisema.

Aidha katika mchezo huo, kiungo wa Azam FC, Mudathir Yahya, anatarajia kurejea tena kikosini mara baada ya kupona majeraha ya ugoko aliyoyapata kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Madini.

Rekodi (H2H)

Timu hizo zitakuwa zikikutana kwa mara ya nne kwenye michuano hiyo, mara tatu zilizopita Azam FC ikiwa na rekodi nzuri ya kupata matokeo dhidi ya Yanga, ikishinda mechi mbili na kutoka sare moja, ikiwa haijapoteza hata moja.

Mara ya kwanza zilikutana mwaka 2012 kwenye hatua ya makundi na Azam FC kuibuka kidedea kwa mabao 3-0, yaliyofungwa na gwiji wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’ kwa mkwaju wa penalti na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Kipre Tchetche, aliyefunga mawili.

Ushindi huo uliiwezesha Azam FC kutinga nusu fainali ya michuano hiyo na kukutana na Simba na kuiadhibu mabao 2-0, yaliyofungwa na Bocco na Gaudence Mwaikimba kabla ya kutinga fainali ikiichapa Jamhuri 3-1.

Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, walikutana na Yanga tena kwenye michuano hiyo mwaka 2016, kwenye mchezo wa hatua ya makundi ulioisha kwa sare ya bao 1-1, Azam FC ikifunga kupitia Tchetche kabla ya Yanga kusawazisha kupitia beki Vincent Bossou.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa mwaka juzi, kwenye hatua ya makundi, Azam FC ikipata ushindi mnono wa mabao 4-0, yaliyowekwa kimiani na Bocco, Joseph Mahundi, Yahaya Mohammed na Enock Atta.

Azam FC ikatinga nusu fainali na kuichapa Taifa Jang’ombe bao 1-0, lililofungwa na Frank Domayo ‘Chumvi’ kabla ya kutwaa taji la michuano ikiichapa Simba 1-0, Himid Mao ‘Ninja’ akiwa mfungaji wa bao hilo.