BAADA ya kucheza dakika 1,440 (sawa na mechi 16) bila kupoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), hatimaye rekodi hiyo ya Azam FC imesitishwa baada ya kufungwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar, mchezo uliofanyika Uwanja wa Manungu, Turiani Morogoro jana Jumamosi jioni.

Azam FC iliyokuwa haijapoteza mechi yoyote ya ligi katika mechi 16 za ligi, ilikuwa ikicheza mechi ya mwisho ya kufunga mwaka 2018 kabla kwenda kutetea taji la michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoanza kutimua vumbi Jumanne ijayo visiwani Zanzibar.

Kufuatia matokea hayo, Azam FC imebakiwa na pointi zake 40 katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi huku ikizidiwa pointi 10 na Yanga inyoongoza kwa pointi 50 lakini ikiwa imecheza mchezo mmoja zaidi ya matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex.

Benchi la ufundi la Azam FC lilikifanyia marekebisho kikosi hicho dhidi ya Mtibwa Sugar, ambapo kwenye eneo la ulinzi alipumzishwa nahodha Agrey Moris na kipa Razak Abalora na nafasi zao kuchukuliwa na David Mwantika na Mwadini Ally.

Kutokana na majeruhi ya viungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya na Joseph Mahundi ambaye pia amekusanya kadi tatu za njano na Danny Lyanga, nafasi zao zilijazwa na Stephan Kingue, Tafadzwa Kutinyu, aliyeshushwa chini kucheza namba nane badala ya 10 na winga Idd Kipagwile.

Mtibwa Sugar ilifunga bao kwenye kila kipindi cha mchezo huo, la kwanza likifungwa na Kelvin Sabato dakika ya 15 huku Ally Makarani, akitupia la pili dakika 81 kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Azam FC, Mwadini Ally.

Safu ya ushambuliaji ya Azam FC chini ya Donald Ngoma na Obrey Chirwa, aliyekuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya ligi tokea asajiliwe kwenye dirisha dogo, ilionekana kupwaya na kushindwa kufanya makeke yao ya kuipatia mabao timu hiyo.

Baada ya mchezo huo, hivi sasa Azam FC inawekeza nguvu zake zote kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambapo inatarajiwa kuelekea Zanzibar kesho Jumatatu mchana tayari kuanza kutetea taji hilo ililolibeba mara mbili mfululizo huku kihistoria ikilitwaa mara nne.

Kikosi cha Azam FC:  

Mwadini Ally, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, David Mwantika, Stephan Kingue/Salmin Hoza dk 80, Idd Kipagwile/Yahya Zayd dk 49, Tafadzwa Kutinyu, Donald Ngoma, Obrey Chirwa, Enock Atta/Ramadhan Singano dk 80