KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kucheza mechi ya mwisho ya kufunga mwaka 2018 kwa kukipiga dhidi ya Mtibwa Sugar, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro kesho Jumamosi saa 10.00 jioni.

Kikosi cha Azam FC kipo kwenye hali nzuri kuelekea mchezo huo, ambapo kimepata fursa ya kufanya mazoezi mara mbili mkoani humo kwenye Uwanja wa Jamhuri na wachezaji wameonekana kuwa na morali nzuri ya kushinda mechi hiyo.

Mabingwa hao wa ligi msimu 2013/2014, hadi sasa wakiwa wamecheza mechi 16 za ligi, ina rekodi bora ya kutopoteza mchezo wowote ikiwa imeshinda mechi 12 na kutoka sare nne, ikiwa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.

Wapinzani wao, Mtibwa Sugar inashika nafasi ya tano kwenye msimamo ikiwa imejikusanyia pointi 23 baada ya kushinda mechi saba, sare mbili na kupoteza mara tano huku nyavu zao zikiwa zimetikiswa mara 11.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amesema kuwa kutokana na nafasi iliyopo timu yake watajipanga na kujaribu kupata pointi tatu.

“Bila shaka Mtibwa Sugar imeondolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, na watataka pia kujionyesha tena, timu ina hali nzuri, wachezaji wana ari ya hali ya juu na hili ni jambo muhimu kama unataka kushinda mechi ya ugenini, unatakiwa kupambana kwa kila mpira, unapokuwa na mpira unausambaza kwa haraka sana na uwanja ni mzuri,” alisema.

Pluijm alisema kuwa kutokana na mechi hiyo kuwa ya mwisho kwa mwaka huu, amejipanga kuwapa zawadi mashabiki wa Azam FC ya kumaliza mwaka huu bila kupoteza mchezo wowote kwa kushinda mtanange huo.

“Tunataka kumaliza mwaka bila kupoteza mchezo na mimi sijaja hapa na timu yangu kwa ajili ya kujilinda, kama unataka kushinda unatakiwa kufunga mabao na unapofunga mabao unatakiwa kufunga bao moja zaidi ya mpinzani wako ili kushinda mechi, kwenda kujilinda sidhani kama ni njia sahihi, unatakiwa kujilinda pale unapotakiwa kujilinda, na kushambulia pale inapotakiwa,” alisema.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwakosa wachezaji wake kadhaa ambao ni majeruhi, mabeki Abdallah Kheri, Daniel Amoah, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya, Frank Domayo ‘Chumvi’, mshambuliaji Danny Lyanga.

Rekodi (Head to Head)

Kihistoria timu hizo zimekutana mara 20 kwenye ligi, Azam FC ikishinda mechi 10, ikipoteza mara mbili na kutoa sare nane, ambapo mchezo wa kesho utakuwa wa 21 kukutana.

Katika rekodi hiyo ya ushindi, Azam FC imeonekana kuwa na uwiano mzuri wa kushinda ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar, ikishinda michezo mara sita kati ya mechi 10 za ugenini, huku imeibuka kidedea nyumbani mara nne.

Mara ya mwisho zilipokutana kwenye Uwanja wa Manungu msimu uliopita, Azam FC ilishinda bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Shaaban Idd, aliyetimkia CD Tenerife ya Hispania.