ZIMESALIA saa chache kabla ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kuvaana na Madini katika mchezo wa raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Jumapili saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC tayari kimemaliza maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo, wachezaji wakiwa kwenye morali ya hali ya juu tayari kufanya vema kwa kuitoa timu hiyo na kusonga mbele kwa raundi ya nne ya michuano hiyo.

Kwa msimu wa tatu mfululizo Azam FC imekuwa na rekodi bora kabisa inapofungua pazia la michuano hiyo kwenye raundi tatu, ambapo imekuwa ikigawa dozi nono kwa timu inazokutana nazo.

Mabingwa hao kutoka viunga vya Azam Complex, kwa mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo, msimu wa 2015/2016 iporudishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) walikutana na African Lyon kwenye raundi hiyo na kuichapa mabao 4-0, yaliyofungwa na kiungo Mudathir Yahya, na wachezaji wa zamani wa timu hiyo, Farid Mussa aliyetupia mawili na Ame Ally aliyefunga jingine.

Msimu uliofuata (2016\2017), Azam FC ilianza patashika ya michuano hiyo kwa kutifuana na Cosmopolitan na kuinyuka mabao 3-1, yaliyowekwa kimiani na gwiji wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’, Shaaban Idd na Joseph Mahundi, aliyefunga la mwisho.

Azam FC ikafanya makubwa tena msimu uliopita (2017/2018), kwa kupata ushindi mnono kwenye raundi ya awali ikiichapa Area C United ya United mabao 4-0, yaliyofungwa na kiungo Salmin Hoza, nahodha Agrey Moris, mshambuliaji Yahya Zayd na winga Enock Atta.

Sasa kinachosubiriwa kesho ni je, Azam FC itaendeleza rekodi yake bora iliyoanza nayo misimu kadhaa iliyopita? Ni jambo la kusubiri.