KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imemrejesha kiungo wake mkabaji Stephan Kingue, kwa mkataba wa mwaka mmoja na kufunga usajili wa dirisha dogo unaomalizika leo Jumamosi saa 5.59 usiku.

Kingue aliyekuwa amepumzishwa mara baada ya kupata majeraha kama ilivyokuwa kwa beki kisiki Daniel Amoah, ambaye naye amerejeshwa kwenye usajili wa dirisha dogo, anarejea akiwa fiti kabisa tayari kuendeleza mapambano.

Aidha mbali na sababu za majeraha, wawili hao waliondolewa kwenye usajili wa dirisha kubwa Julai mwaka huu ikiwa ni kabla ya Azam FC kupata uhakika wa sheria ya kusajiliwa wachezaji 10 wa kigeni msimu huu, ambapo awali tulidhani ingeendelea ya ile ya wachezaji saba.

Ujio wake ni sehemu ya kuimarisha eneo la kiungo cha ulinzi hasa baada ya Nahodha Msaidizi, Frank Domayo ‘Chumvi’, kuwa nje ya dimba kwa muda mrefu akiuguza majeraha ya goti, hivyo kwa sasa atakuwa akisaidiana na viungo wa eneo hilo waliopo Mudathir Yahya na Salmin Hoza.    

Usajili wa nyota huyo kutoka Cameroon unafikisha idadi ya wachezaji tisa wa kigeni waliokuwa kwenye kikosi cha Azam FC, kipa Razak Abalora (Ghana), mabeki Yakubu Mohammed, Daniel Amoah (Ghana), Bruce Kangwa (Zimbabwe), Nickolas Wadada (Uganda), winga Enock Atta (Ghana) na washambuliaji Obrey Chirwa (Zambia), Tafadzwa Kutinyu, Donald Ngoma (Zimbabwe).