BEKI kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Abdallah Kheri maarufu kama Sebo, amefanyiwa upasuaji wa goti nchini Afrika Kusini leo Ijumaa asubuhi.

Kheri amefanyiwa upasuaji huo baada ya kupata majeraha kwenye mchezo wa awali wa timu ya vijana ya Azam FC (Azam B), aliyokuwa akiichezea ili kujiweka fiti baada ya kutoka kuugua malaria, ambapo alidondokea mguu vibaya wakati alipokuwa akitoka juu kuokoa mpira.

Daktari wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankemwa, aliyeambatana naye kwenye matibabu yake nchini humo, amesema kuwa upasuaji wa mchezaji huyo umemalizika salama katika Hospitali ya Vincent Pallotti jijini Cape Town.

“Upasuaji umeenda salama, tutakuja kumuona Dr. Nicholas Jumanne ijayo saa nne asubuhi, na siku hiyo tutaelekezwa programu ya matibabu yake (rehabilitation program) Inshallah Jumatano (19/12/2018) tutarejea nyumbani,” alisema.

Ripoti kamili ya atakuwa nje kwa muda gani pamoja na mambo mengine ya matibabu yake, yanatarajia kuwekwa wazi mara baada ya Mwankemwa kuonana na mtalaamu huyo.

Daktari huyo wa muda mrefu wa tiba za wachezaji, alichukua fursa kutoa shukrani kwa Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo kwa kufanikisha matibabu ya beki huyo, ambaye alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Azam FC mwezi Septemba msimu huu baada ya kuonyesha kiwango bora kabisa.