KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imepangwa kuanza raundi ya tatu ya msimu mpya wa michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Katika droo hiyo iliyofanyika leo Jumatano kwenye ofisi za wadhamini wa michuano hiyo, Kampuni ya Azam Media, imeonyesha kuwa Azam FC itaanzia nyumbani (Azam Complex) kwa kuchuana na mshindi wa mechi ya raundi ya tatu kati ya Madini ya Arusha na Stand Babati, mchezo ambao utapangiwa siku ya kufanyika na waandaaji wa michuano hiyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Hii ni nafasi nyingine kwa Azam FC kurejea kwenye michuano ya kimataifa baada ya kuwa nje kwa miaka miwili, kwani bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao wa michuano ya klabu ya CAF unaoanza Novemba mwakani.

Msimu uliopita Azam FC iliishia hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya kuteleza ikifungwa na Mtibwa Sugar kwa changamoto ya mikwaju ya penalti, 9-8 baada ya dakika 90 za kawaida za mchezo kumalizika kwa suluhu.

Historia ya Azam FC kwenye michuano hiyo iliyofikisha msimu wa nne, iliwahi kufika fainali msimu wa kwanza na kufungwa na Yanga mabao 3-1 kabla ya msimu uliofuatia kuishia nusu fainali ikifungwa na Simba bao 1-0 na msimu wa tatu ikitolewa na Mtibwa Sugar.