KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imelazimisha sare ya mabao 2-2 ugenini dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Sare hiyo inaifanya Azam FC kuendelea kusalia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa imefikisha pointi 40 ikizidiwa pointi moja na Yanga iliyo kileleni kwa pointi 41, ambayo ina mchezo mmoja mkononi.

Azam FC haikuwa kwenye kiwango chake bora kilichozoeleka, ilijikuta ikitanguliwa kufungwa bao la kwanza dakika ya 18 likifungwa na George Sangija, baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa timu hiyo.

Kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu, aliisawazishia Azam FC dakika ya 45 kwa shuti la kiufundi akimalizia krosi safi ya chini ya winga Enock Atta, aliyemzidi maaraifa beki wa KMC, Kelvin Kichiri, na hilo linakuwa bao la tano kwa Kutinyu kwenye TPL msimu huu.

Kipindi cha pili Azam FC ilirejea kwa kasi ikitaka kupata bao la ushindi lakini umakini ulionekana kupotea kwa washambuliaji kwa kupoteza nafasi za wazi.

KMC ilijipatia bao la pili dakika ya 63 likifungwa na Rayman Mgungila, aliyemalizia mpira uliotemwa na kipa wa Azam FC, Razak Abalora, akipangua shuti lililopigwa na Rehani Kibingu.

Azam FC iliendelea kuleta kashikashi langoni mwa KMC na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 85 lililofungwa na mshambuliaji Donald Ngoma, akimalizia pasi safi ya juu ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, likiwa ni bao lake la nne msimu huu.

Mshambuliaji Danny Lyanga, angeweza kuipatia ushindi Azam FC baada ya kukosa nafasi nzuri kuelekea mwisho wa mchezo huo, baada ya kupewa pande safi na Sure Boy kabla ya kuingia kwenye eneo la hatari pembeni na kupiga shuti lililomlenga kipa.

Sare hiyo inaifanya Azam FC kutibuliwa rekodi yake ya kushinda mechi tisa mfululizo za ligi, ambapo hadi sasa ikiwa imecheza mechi 16 za ligi, imefanikiwa kushinda mechi 12 na sare nne ikiwa haijapoteza mchezo wowote.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Hassan Mwasapili, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya, Joseph Mahundi/Yahya Zayd dk 62, Salum Abubakar, Donald Ngoma, Tafadzwa Kutinyu/Danny Lyanga dk 79, Enock Atta/Ramadhan Singano dk 79